Hili Ndilo Tatizo la Wasanii wa Kike
UKIMWULIZA msanii wa kike anakutana na changamoto gani kwenye kazi yake ya sanaa, pamoja na nyingine wengi watakutajia kusumbuliwa kimapenzi.
Naomba niweke wazi mapema, kuna tofauti kati ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na kutakiwa kutoa rushwa ya ngono. Hapa nazungumzia usumbufu wa rushwa ya ngono.
Hiyo imekuwa kero kubwa kwa wasanii wa kike. Utakuta msanii ana kipaji kikubwa sana cha kuigiza, lakini anakutana na kikwazo hiki. Hakuna kupewa roll kubwa kwenye muvi mpaka atoke na director.
Kwenye muziki kilio ni hichohicho. Msanii anahangaika kufanya mazoezi, anasaka pesa ya kurekodi na kwenda studio. Akifika huko anaweza kukutana na prodyuza mroho akamsumbua.
Asipokutana na mtayarishaji msumbufu basi kuna kikwazo kwa staa anayetaka kumshirikisha kwenye ngoma yake. Mwanzo atajifanya ana lengo la kumsaidia kwenye singo yake tena bila malipo yoyote.
Watakutana, watashirikiana kuandika mistari, watafanya mazoezi pamoja nk, lakini ikifika siku ya kuingiza vocal ataanza visingizio na mwisho wa siku atataka kutoka na msanii husika.
Akipenya hapo, ngoma ikitoka atakutana na watangazaji wenye tabia hizo na huko watamwekea kauzibe. Akiona inakuwa ngumu, anaweza kuamua kwenda kwenye magazeti – atakutana na mambo hayohayo.
Kama sivyo basi atatakiwa atoe fedha. Hapo ndiyo unakuwa mwisho. Stori ni hiyohiyo hata kwenye filamu. Msanii anacheza filamu moja, kisha ndiyo imetoka.
Asilimia kubwa ya waliongia kwenye mkumbo wa namna hiyo wameishia pabaya. Wamepoteza nafasi za kutoka na vipaji vyao pia vimefia hapo.
Lakini pamoja na changamoto hiyo kuwa kikwazo na kuwarudisha nyuma wasanii wa kike tatizo kubwa ni kutojiamini.
Orodha ya wasanii wa kike walioamua kuachana na sanaa au sanaa kuwaacha baada ya kudanganyika ni ndefu, nawapongeza sana wale waliojitahidi na kushikilia misimamo yao.
Wapo wasanii wa mfano ambao tunao kwenye sanaa na mpaka sasa wanafanya vizuri. Lady Jaydee ni miongoni mwao. Alianza kuvuma mwaka 2000 (miaka 17 iliyopita) na mpaka sasa yupo kwenye game.
Hebu jiulize, wasanii walioanza muziki na Stara Thomas waliishia wapi? Wako wapi walioingia kwenye uigizaji na kina Monalisa, Thea na Johari? Tatizo ni kutojiamini.
Wasanii wa kike msikubali kutumiwa na waroho, wasio wastaarabu na wasioheshimu thamani ya mtoto wa kike. Mkijiamini na kushikamana mtaweza kushinda kizingiti hicho.
Gazeti la Mtanzania