Mzee Majuto Afungukia Ombi Lake Kugonga Mwamba kwa JK
Msanii mkongwe wa vichekesho nchini Tanzania, Amir Athuman maarufu kama Mzee Majuto amesema amegundua jambo lililopelekea kunyimwa kununuliwa trekta na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni kutokana na kuomba kama mtu binafsi na wala siyo kwa kikundi maalum.
Mzee Majuto amebainisha hayo hivi karibuni baada ya kupita takribani miaka minne alipoomba kufanyiwa kupitia kipindi cha Mkasi kilichokuwa kinarushwa na tinga namba kwa vijana EATV , ambapo Kabla ya kipindi kufungwa Majuto aliomba nafasi ya kuwasilisha jambo lake kwa Rais wa awamu hiyo kwa kusema ‘kama Mhe. Rais ananisikiliza, namwomba aninunulie gari ya kulimia ili na mimi niweze kupata walau kulima nikiwa mapumzikoni huko nyumbani, kwani ndoto yangu ni kuja kufanya kilimo ni kiacha kazi hii ya sanaa’.
“Najua kosa ambalo nimelifanya mpaka nimekosa trekta nililoomba kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni kwa sababu niliomba kama mimi lakini tungeomba kama kikundi chenye watu 10 au 15 tungeweza kusaidiwa na Mhe. kutokana anapenda kusaidia wengi siyo mmoja mmoja”, amesema Mzee Majuto.
Kwa upande mwingine, Mzee Majuto amesema kazi yake ya sanaa imeweza kumsaidia katika kumuinua kiuchumi tokea alipoanza mpaka leo hii huku akijidai kuwa hana wasiwasi juu ya namna gani anapata ugali.