CD na DVD 7,780 Bandia Zakamatwa Dar
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata CD na DVD 7,780 za muziki na filamu kutoka kwa wasambazaji mbalimbali jijini Dar es Salaam zikiwa bila stempu za kulipia kodi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Zoezi hilo liliendeshwa kwa kushirikiana na Kampuni ya Yono Auction Mart na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali, ambapo lilibaini ukiukwaji huo wa sheria katika kazi za wasanii unaofanywa na baadhi ya wasambazaji.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, alisema msako huo uliofanyika mwishoni mwa wiki ulibaini udanganyifu mwingine wa kutumia stempu kinyume na sheria unaofanywa na wasambazaji hao.
“Kuna baadhi ya wasambazaji wameibua tabia ya kuweka CD au DVD mbili kwenye kasha moja, huku nakala moja ya CD au DVD ikiwa imebandikwa stempu halali ya kodi na nakala nyingine haina stempu pia nyingine tulizokamata stempu zake zilikuwa zimeskaniwa badala ya kubandika stemp halali kisheria,” alieleza Kayombo.
“TRA inatoa wito kwa wasambazaji wote wa kazi za wasanii kutumia stempu za kodi kwa mujibu wa sheria na tunasisitiza kwamba ni sharti wahusika wanaoingiza kazi za wasanii kutoka nje ya nchi wapate kibali kutoka Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili wapate kibali cha kubandika stempu kwenye kazi hizo na si vinginevyo,” alisema Kayombo.
Mtanzania