Shetta Atumia Ndege, Boti Kwenye Video Mpya
VIDEO ya wimbo mpya wa ‘Namjua’ wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nurdin Bilali ‘Baba Qayla’ au ‘Shetta’, iliyorekodiwa katika miji ya Johannesburg na Cape town nchini Afrika Kusini, inatarajiwa kuachiwa kesho katika vituo mbalimbali vya runinga.
Uwekezaji katika video hiyo umekuwa mkubwa kwani zimetumika ndege, boti na nyumba za kukodi zilizogharimu kiasi kikubwa cha fedha ili kuvutia na kujiongeza katika soko la kimataifa.
Shetta alisema ametumia siku nne kurekodi wimbo huo baada ya wiki mbili za kusaka na kupata mandhari nzuri zinazoonekana katika video hiyo.
“Video hii nimewekeza vya kutosha maana hadi wasichana ‘video queens’ waliotumika humo ni wa kimataifa. Video yenyewe inaelezea mambo mbalimbali ikiwemo mapenzi na ufahari katika mambo mbalimbali, imani yangu itanifikisha kimataifa zaidi,” alieleza Shetta.
Video hiyo imerekodiwa chini ya studio ya WCB na mtayarishaji kutoka kisiwani Comoro, Jobanjo akishirikiana na prodyuza, Laizer kutoka studio hiyo.
Mtanzania