-->

Haya Ndiyo Yaliyobamba 2015

MWAKA2015

Unaweza kuuelezea 2015 kama mwaka wa pilika nyingi kutokana na kuwapo kwa matukio mbalimbali katika nyanja za kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.

Imeshuhudiwa shughuli kadhaa katika siasa kama vile Uchaguzi Mkuu, lakini kwa upande wa kijamii hususan burudani, yapo mambo mengi yaliyotokea pengine kuweka historia katika tasnia hiyo.

Tuzo kwa wasanii

Mchango wa wasanii wa Tanzania umeendelea kutambuliwa na mataifa mbalimbali duniani baada ya baadhi ya wasanii kujizolea tuzo mbalimbali ndani ya mwaka huu.

Mwanamuziki Naseeb ‘Diamond’ Abdul ameibuka kinara kwa kupokea tuzo nyingi zaidi. Baadhi ya tuzo alizoshinda ni pamoja na All Africa Music Awards (Afrima) zinazotolewa na MTV Base, MTV Europe zilizofanyika jijini Millan Italia, Nafca za Nigeria. TTTM kutoka Burundi, Abryanz kutoka Uganda lakini pia Africa Music Magazine Awards Afrimma zilizotolewa Texas Marekani.

Wasanii wengine walitambuliwa michango yao nje ya nchi ni pamoja na Ali Kiba, Vanessa Mdee, Ommy Dimpoz na kwa upande wa tasnia ya mitindo kwa mwaka huu, Millen Magesse na Flaviana Matata bado wanafanya vizuri kimataifa huku Martin Kadinda, Rio Paul, Ally Daxx na Hariet Paul wakifanya vizuri kwa upande wa Afrika.

Kwa upande wa tuzo za ndani kwenye sanaa waliochukua tuzo ni pamoja na Ally Kiba aliyezoa tuzo tano za muziki kupitia tuzo za Kilimanjaro, wengine ni Vanesa Mdee, Jose Mara, Mzee Yusuf, Joh Makini Isha Ramadhani , lakini pia wako wasanii waliong’ara katika filamu na kutambuliwa michango yao kupitia wadau kadhaa.

Jokate Mwegelo na Ernest Napoleon wakipata tuzo za (ZIFF)

Matamasha

Ukiacha tuzo katika tasnia ya muziki, mwaka 2015 ulipambwa na matamasha kadhaa ambayo yalitoa fursa kwa Watanzania na watu wa mataifa mbalimbali kushuhudia na kuonyesha vipaji vyao na ubunifu.

Sauti za Busara

Likifanyika kwa mara ya 12 tangu kuanzishwa kwake, tamasha hili la kimataifa lililofanyika katika Viwanja vya Ngome Kongwe Kisiwani Unguja, liliwaleta pamoja zaidi ya wasanii 400 kutoka nchi 20 duniani. Wasanii hao walijumuika pamoja na wageni wengine kwa muda wa siku nne wakibadilishana uzoefu katika tasnia ya muziki na sanaa za maonyesho. Hili lilikuwa Tamasha kubwa la kwanza lililotangulia na lilifanyika Februari.

Tamasha la Filamu la Zanzibar (ZIFF). Hili nalo lilifanyika kisiwani Unguja, likiwakutanisha wasanii wa filamu na utamaduni kutoka nchi mbalimbali. Liliambatana na warsha na makongamano yanayohusu tasnia hiyo kisha kufuatiwa na tamasha hilo. Tamasha hilo lilihitimishwa kwa kutambua michango ya waigizaji na wadau mbalimbali kupata tuzo. Zaidi ya tuzo 12 zilitolewa.

Tamasha la karibu

Hili lilikutanisha zaidi ya vikundi 30 kutoka ndani na nje ya nchi. lililifanyika katika viunga vya Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Wasanii wakubwa na wachanga nchini walipata wasaa wakujumuika pamoja kubadilishana uzoefu katika fani hiyo ya muziki. Tamasha hilo lilihitimishwa kwa burudani kutoka kwa mwanamuziki Papa Wemba kutoka Kongo.

Ujio wa wanamuziki kutoka nje

Mwaka huu tumeshuhudia ujio wa wanamuziki mbalimbali akiwamo mwanamuzi Koffi Olomide anayetamba na kibao chake cha ‘Selfie’ lakini pia mwanamuzi na mtangazaji kutoka Zambia, Roberto Banda aliyepiga wimbo wa ‘Amarula’.

Maonyesho ya mavazi

Hata hivyo, idadi ya maonyesho ya mavazi imeonekana kupungua tofauti na mwaka jana, kuna baadhi ya maonyesho makubwa yaliyozoeleka kufanyika kila mwaka hayakufanyika kabisa.

Baadhi ya maonyesho ya mavazi yaliyofanyika kwa mwaka huu ni pamoja Fashion Night Out lililoandaliwa na mbunifu Doreen Mashika kutoka Zanzibar. Mbali na onyesho hilo, mbunifu Mustafa Hassanali alikuja na onyesho la kimataifa la Swahili Fashion Week, lililowaleta pamoja wabunifu wa mitindo, wanamitindo na wadau mbalimbali wa tasnia hiyo ulimwenguni.

Onyesho la kusaka vipaji (BSS)

Hili pia lilikuwa gumzo kwa wapenzi na wadau wa muziki nchini. Vipaji vilitafutwa katika kanda zote nchini na hatimaye kupatikana mshindi aliyejizolea mamilioni ya shilingi.

Watanzania walipata wasaa wa kushuhudia na kupiga kura kumchagua mshindi. Shindano lilikuwa na msisimko zaidi tofauti na miaka iliyotangulia.

Wimbi kubwa la wasanii kujiingiza kwenye siasa

Ilikuwa ni kawaida kuona wasanii wakijihusisha kwenye siasa kwa kutumbuiza, watu wanaofika kwenye maeneo ya kampeni. Lakini kwa mwaka huu mambo yamekuwa tofauti, kwani wimbi kubwa la wasanii liliingia kwenye kampeni za uchaguzi wakiwa na lengo la kupata ridhaa ya wananchi kuongoza. Katika mchakato huo wapo waliofanikiwa na wengine walioanguka. Wasanii waliofanikiwa ni pamoja na Joseph Haule aliyeshinda ubunge lakini pia baba Levo na Said Fela walioshinda udiwani.

Waliojaribu ni pamoja na Wema Sepetu, Jackine Wolper, Rashid Mwinshehe na Wastara Juma.

By Maimuna Kubegeya, Mwananchi

Comments

comments

Post Tagged with

Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364