Mastaa Waliobadili Dini Kisa Ndoa, Watumbuliwa
Baadhi ya wasanii wa filamu Bongo waliowahi kufanya uamuzi wa kubadili dini kutoka kwenye Ukristo kuingia kwenye Uislam ‘wametumbuliwa’ kufuatia mienendo yao isiyokubalika.
Masupastaa hao wakiwemo Jacqueline Wolper, Rose Ndauka, Flora Mvungi, Aunt Ezekiel na Ester Kiama wametumbuliwa kutokana na kutoonesha jitihada zozote za kuijua vilivyo dini waliyoiendea.
Akizungumza na Ijumaa, hivi karibuni, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum alisema kuwa, kitendo cha mtu kubadili dini kisha kutoonesha utofauti hakuna maana na ni bora kubaki kwenye dini ya awali.
“Kwanza wanaokosea ni wale wanaowasilimisha maana wakishawabadili dini hawafanyi jitihada za kuwatafutia watu wa kuwafundisha misingi ya Dini ya Kiislam, matokeo yake sasa unakuta mtu amebadili dini na kupewa jina la Kiislam lakini hafuati misingi ya dini.
“Lakini pili, hawa wanaobadili dini wenyewe hawaoneshi kutaka kujifunza, wanaridhika na ile hali ya kuambiwa wamesilimu na kupewa majina mazuri ya Kiislam lakini baada ya hapo wanabaki walewale,” alisema shehe huyo.
Wolper, Rose, Flora, Aunt na Ester ni kati ya wasanii wa Bongo waliosilimu huku baadhi yao wakifanya hivyo kufuata imani za wachumba zao ili waolewe lakini mpaka sasa hakuna aliyeonesha utimilifu wa kusilimu kwake, badala yake baadhi yao wameendelea na mifumo yao ya maisha kama walivyokuwa wakiishi walipokuwa Wakristo.
Chanzo:GPL