‘Bifu’ la Diamond, Kiba Linalipa
MOJA ya mbinu inayotumiwa na nyota mbalimbali wa muziki duniani ni ile ya kutengeneza bifu bandia na kuwahusisha mashabiki wao. Mbinu hiyo inasaidia kuuza idadi kubwa ya nakala za kazi za sanaa za wasanii hao wenye bifu.
Asikwambie mtu! Hapo ndipo wasanii wengi wanapiga hela. Wakati mashabiki wanatupiana vijembe vilivyojaa kejeli za hapa na pale kuhusu bifu hilo bandia, ndiyo kazi za wasanii hawa zinapopata nafasi sokoni.
Hali hiyo inafanya wasanii wengine na kazi zao kutopewa nafasi ya kujadiliwa kama wanavyojadiliwa wasanii waliopo kwenye bifu hilo bandia lenye lengo kuwanufaisha kibiashara na mara nyingi uhodari wao wa kuunda bifu hufanya mashabiki wasijue kama ni bifu kweli au ni bifu la magumashi.
Ukiizungumzia Bongo Fleva hivi sasa akili yako moja kwa moja itagota kwa vijana wawili, Ali Kiba na Diamond Platnumz. Sababu inayofanya uwafikirie wasanii hao ni kile kinachoitwa bifu lililochukua miaka minne na zaidi sasa.
Hapo ndiyo unaona Ali Kiba akifanya vyema kwenye biashara yake ya muziki na Diamond Platnumz akinufaika vilivyo na bifu hilo pale anapotoa kazi mpya.
CHANZO CHA BIFU LAO
Watu wao wa karibu wanasema chanzo kilianza mwaka 2012 pale ambapo Diamond alitakiwa ashiriki kwenye wimbo wa Single Boy ulioimbwa na Ali Kiba.
Lakini haikuwa hivyo kwani nafasi ya Diamond aliichukua Lady Jay Dee, kitendo kilichomchukiza Diamond na kufikia hatua ya kufuta sauti ya Ali Kiba kwenye wimbo aliomshirikisha.
WADAU WAWATULIZA
Unaweza ukashangaa ishu ndogo kama hiyo imewezaje kufanya wawili hawa wawe kwenye bifu mpaka leo hii. Washkaji zao wa karibu wanasema mara nyingi watu wenye heshima kwenye muziki huu wamewaita na kuwapatanisha bila jitihada hizo kuzaa matunda kwani tayari faida ya bifu lao walianza kuziona.
Hata pale wadau wakuu wa muziki huu walipofanikiwa kupunguza makali ya hasira zao, walishindwa kuzuia hasira ya uzalendo iliyojengeka kwenye mioyo ya mashabiki wao waliotengeneza timu zenye nguvu yaani Team Kiba na Team Diamond.
KAZI KUBWA ZA TIMU
Baada ya mashabiki kuunda timu sasa ni mwendo wa kushindana na kukomoana. Kazi ya timu ni kuhakikisha msanii wao anapotoa audio au video basi timu ni lazima ipigane ihakikishe inafika mbali.
Diamond akitoa audio au video basi mashabiki wa Ali Kiba watatumia mapungufu yaliyopo kwenye kazi hiyo, kukosoa ngoma ya Diamond, kadhalika kwa Ali Kiba. Kumbuka wakati mashabiki wa Diamond wanaiponda kazi ya Ali Kiba, mashabiki wa Ali Kiba wanaitetea na kufanya mjadala mzito kuibuka na kugonga vichwa vingi vya habari.
Kiukweli wamefanikiwa na ndiyo maana kama wewe ni msanii ukitoa wimbo siku moja na Diamond au Ali Kiba, basi kazi hiyo haitafika popote itakufa mapema iwezekanavyo.
MAPENZI YANOGESHA BIFU
Diamond aliwahi kutoka kimapenzi na Jokate Mwegelo. Inasemekana hivi sasa Jokate anatoka na Kiba. Mashabiki hawakosi neno kwani wale mashabiki wa Diamond watauponda uhusiano wa Kiba na Jokate kadhalika wa Kiba wanauponda uhusiano wa Diamond na Zari kwa kigezo cha kuzidiana umri.
Mrembo yeyote aliyewahi kutoka na Diamond, akionekana amepiga picha na Ali Kiba basi habari yake siyo ndogo hapa mjini, mfano ni Wema Sepetu.
SHOO, MATUKIO YA KIJAMII
Mashabiki wa Diamond wapo tayari kulipa kiingilio ili wakaharibu onesho la Ali Kiba, hivyohivyo Diamond anapata sana shida anapokutana na nyomi lililojaa mashabiki wa Ali Kiba, tujikumbushe kwenye Fiesta 2014 pale Leaders Club.
Juzi kati hapa Diamond alikwenda kusaidia watoto wenye ugonjwa wa mgongo wazi na vichwa vikubwa, habari ikawa kubwa zaidi pale Ali Kiba naye alipokwenda kutoa msaada wa milioni 21 zaidi ya Diamond aliyetoa milioni 20.
SIKIA HII
Mfano leo hii Ali Kiba na Diamond Platnumz wanamaliza tofauti zao, wakapeana mikono na kufanya kazi pamoja, wewe shabiki utakuwa na hamu ya kuendelea kuwafuatilia?
Na ujue kuwa wewe shabiki usipotia mzuka wako na biashara yao ya muziki inayumba na tunaweza kuwapoteza kabisa wawili hawa.
Hapo ndipo ninaposema bifu hili ndiyo uhai wa biashara yao ya muziki. Wakija kupatana hakuna cha Chibu Dangote wala King Kiba, huo utakuwa mwisho wa zama zao.
Mtanzania