Kanumba, Tyson, Kuambiana… Wameondoka na Soko?
BADO naendeleza kelele zangu kwenye soko la filamu nchini ambalo kwa sasa limedorora na kama hatua za makusudi hazitachukuliwa basi kuna hatari ya kupotea kabisa.
Wadau wa sanaa wale wanaoitakia mema tasnia ya filamu, wanapiga kelele kurudisha heshima ya sanaa na wasanii wa filamu Tanzania.
Zipo hoja nyingi zinazowekwa mezani. Hata wiki iliyopita nilijenga hoja kadhaa kuhusu kushuka kwa filamu zetu, nikieleza kuwa zaidi ni maudhui, ushindani na usambazaji.
Niseme wazi tu kwa mara nyingine, pamoja na kwamba yapo mengi, lakini chanzo kikuu ni utaratibu mbovu wa usambazaji.
Wengine wanajenga hoja kuwa, filamu zimepoteza mvuto baada ya kifo cha staa wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba. Wengine wanadai hata kuondoka kwa waongozaji wenye vipaji, Adam Kuambiana na George Tyson ni sababu ya kutoka filamu mbovu.
Inaweza kuwa hoja nzuri zaidi kama ikielezwa kuwa, tasnia ya filamu imeanza kupoteza mvuto katika kipindi ambacho mastaa hao wamefariki dunia.
Hebu jiulize; je, ni kwamba marehemu Kanumba ndiye pekee alikuwa mkali wa filamu za Kitanzania? Mtazame kwa mfano msanii Mohamed Mwikongi ‘Frank’, hivi unaweza kusema siyo msanii mzuri?
Hemed Suleiman, Jacob Stephen ‘JB’, Yusuph Mlela, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Suleiman Barafu, Mzee Almasi, Single Mtambalike ‘Richie’ na wengineo; ni kweli hawa wote siyo wasanii wazuri?
Jibu ni moja tu, siyo kweli. Kanumba alikuwa na ladha na staili yake ya peke yake, huku wasanii wengine wakitamba kwa staili zao kivyao pia. Kila mmoja ana ladha yake.
Hoja kwamba Kanumba ameondoka na filamu zake, naweza kusema haina mashiko, lakini nitakubali kuwa katika kipindi hiki ambacho marehemu Kanumba ameondoka, kuna mdororo mkubwa wa soko la sinema nchini.
Marehemu Kanumba kwa kujua kuwa hakuwa mkamilifu, ndiyo maana alikuwa akishirikiana na wasanii wengine katika kazi zake. Kanumba amecheza na wasanii wengi sana, maarufu na chipukizi.
Pamoja na ukali wake, hakusita kushirikiana na Ray katika baadhi ya filamu baada ya kila mmoja kuwa na kampuni yake. Baadhi ya sinema hizo ni pamoja na O’prah na Off Side ambazo mpaka sasa zinafanya vizuri. Lengo lilikuwa kuchanganya ladha na kuvuta mashabiki zaidi.
MADINI YA KANUMBA
Kiu ya Kanumba ilikuwa kufanikiwa kwake kisanii lakini pia kwa industry nzima ya Bongo Movies. Kazi za Kanumba siku zote hazikuwa za kubabaisha, ni kama ilivyo kwa Ray, JB na wasanii wengine ambao bado wanajitahidi kufanya vizuri.
Ile kiu ya Kanumba ya kuingia kwenye ushindani wa soko la kimataifa ikiwaingia wasanii wetu, tunaweza kusogea mbele zaidi. Kumbuka kwamba, nilisema mchawi mkuu ni msambazaji, lakini angalau basi tuanze na kazi nzuri.
ADAM KUAMBIANA
Marehemu Kuambiana, naye alikuwa na mchango mkubwa kwenye sanaa. Huyu alikuwa zaidi ya mwigizaji – alikuwa mkali katika kutunga hadithi, kuandika miswada na kuongoza.
Bahati nzuri niliwahi kufanya naye kazi, hivyo naweza kuelezea uzuri wake katika hilo kikamilifu. Ametia mkono katika filamu nyingi za JB na naweza kusema JB ndiye aliyevumbua kipaji chake cha kuongoza ambacho wengi hawakukijua kabla.
Kuna ya kujifunza kutoka kwake. Pengine waandishi, waongozaji na watayarishaji wanaweza kuchukua vitu kupitia kazi zake.
Hata hivyo, watayarishaji wa sasa hawana ushindani, wanataka vitu vya rahisi. Mfano sioni mwandishi mashuhuri Ally Yakuti akitumika kwenye filamu nyingi za siku hizi.
Najua Yakuti ni professional na hapokei malipo ya ubabaishaji ndiyo maana wanamkimbia.
Filamu haziwezi kuwa bora kama hatutawekeza. Wapo wengi wenye kariba ya Yakuti lakini hawapewi kazi kwa kuogopa kuwalipa. Tutaendelea kusubiri sana treni airport!
GEORGE TYSON
Alikuwa mwongozaji wa aina yake. Amefanya kazi nyingi za filamu ikiwemo sinema ya mwanzo kabisa kuchomoza kwenye tasnia ya filamu za kisasa – Girlfriend ambayo aliwachezesha wasanii wa filamu na muziki.
Kipaji, ubunifu na uwezo wa kupanga wasanii wanaotakiwa na mswada ndiyo uliomfanya awe mwongozaji wa kipekee. Waongozaji wetu wanaweza kuendeleza yale aliyokuwa akiyafanya ili kupata filamu nzuri wakati tukiendelea kutafakari usambazaji wa uhakika.
TUACHE KULALAMIKA
Kuendelea kulalamika kuwa soko limepoteza mvuto bila kutafuta mbinu za kuliokoa, hakuna maana. Tutafute dawa kwa kufuata, pamoja na mengine mengi, hayo niliyoeleza hapo juu.
Nasisitiza: Hatuweza kudharau mazuri yaliyofanywa na wapendwa wetu waliotangulia, lakini kuyaenzi na pengine kukazana zaidi yao ili sanaa ya filamu zetu irudi kwenye chati.
Mtanzania