Alikiba Afurahia Kuwepo Coke Studio
MKALI wa muziki wa Bongo Fleva nchini, Ali Kiba, amesema moja ya mafanikio ambayo anajivunia kwa mwaka huu ni kushiriki tena onyesho la Coke Studio.
Kiba, ambaye amefanya kolabo na mwimbaji wa Nigeria, Patoranking, amesema kushiriki msimu huu wa tano wa Coke Studio kutamfanya aongeze idadi kubwa ya mashabiki.
“Kushiriki katika onyesho hili linaloandaliwa na kampuni kubwa ya vinywaji ya Coca Cola pamoja na kushirikiana na Patoranking, kunanifanya niongeze mashabiki na umaarufu wangu kuongezeka,” alisema Kiba.
Alisema onyesho la Coke Studio linadhihirisha kuwa Bongo Fleva inazidi kukua na kupata umaarufu sehemu mbalimbali barani Afrika kutokana na jinsi linavyofuatiliwa na idadi kubwa ya mashabiki.
Pia Kiba aliwapongeza wasanii wenzake kutoka Tanzania ambao wamepata nafasi ya kushiriki onyesho hilo la Coke Studio linaloonyeshwa kila Jumamosi kwenye televisheni ya Clouds, ambapo wasanii hao ni Rayvanny, Izzo Bizness na Nandy.