Baba mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Mzee Abdul Juma alipofika getini kwenye studio ya Diamond.
Na Musa Mateja Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Abdul Juma ambaye ni baba mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ amenaswa akiwa katika studio ya mwanaye iliyopo Sinza Mapambano jijini Dar akidaiwa kusaka suluhu ya ugomvi wake na mwanaye, Risasi Jumamosi lina habari kamili.
Katika kusaka suluhu ya ugomvi wao huo wa muda mrefu, chanzo kilieleza kuwa, mzazi huyo hakujali ugonjwa wa miguu unaomsumbua kwa muda mrefu, kwani alikuwa tayari hata kufia studioni hapo ilimradi afanikiwe kuonana na Diamond, wamalize tofauti zao.
TUJIUNGE NA CHANZO
Februari 10, mwaka huu, mwanahabari wetu alipokea simu iliyoeleza kuwa mzazi huyo alikuwa akimsaka Diamond ambapo alilazimika kuweka makazi ya muda kwenye jengo lililo studio hiyo huku akiwa mgonjwa, akiwa na lengo moja tu, kumaliza tofauti zao.
“Njooni hapa Mapambano kwenye studio ya Diamond, baba Diamond amefika hapa, anaonekana mgonjwa hata tembea yake anazunguka hapa mara atoke geti hili, mara aende lingine maana nyumba hii ya studio ina mageti mawili.
“Anasema bora afie hapa lakini lazima leo aonane na Diamond ili moyo wake uridhike. Ameongozana na mwanaume mmoja nafikiri ndiye anayempa msaada wa karibu,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata maelezo hayo kutoka kwa chanzo, mwanahabari wetu kwa kutumia usafiri wa bodaboda, alifika fasta katika studio ya Diamond na kumkuta mzee huyo aliyeonekana kuumwa miguu iliyokuwa imevimba, akihaha kugonga geti la nyumba hiyo ya studio.
Kwa kutumia kamera za kidaku zaidi, mwanahabari wetu alikita kambi maeneo ya jirani na studio hiyo tangu saa 5 asubuhi hadi jioni akisubiri kuona namna itakavyokuwa wawili hao watakapoonana, huku akimfotoa picha tofauti mzazi huyo na mpambe aliyeongozana naye.
WACHOKA, WAKAA
Kuna wakati mwanahabari wetu alimshuhudia baba Diamond na mwenzake wakiwa wamechoka kugonga mageti ya nyumba hiyo na kuamua kukaa chini katika mawe yaliyokuwa jirani.
“Mzee anaonekana anaumwa yule, ona anavyokaa pale anaonekana ana maumivu mwilini ila atakuwa anajikaza tu, si bora angepumzika tu nyumbani akatafuta njia mbadala ya kuonana na Diamond,” alisikika shuhuda mmoja.
RISASI LAMVAA BABA DIAMOND
Baada ya kumfotoa picha za kutosha, Risasi Jumamosi lilimfuata mzazi huyo na kumuuliza kulikoni afike studio hapo angali mgonjwa na kwa nini asiwasiliane na mwanaye kwenye simu? Mzee huyo alifunguka:
“Yametokea mengi huko nyuma, lakini nahisi ni muda muafaka wa kumaliza hizi tofauti zetu. Katika pitapita zangu maeneo haya, nikaoneshwa hapa ndiyo studio kwake, nikaona bora nishinde hapa kutwa nzima nikiamini lazima atafika tu japo naumwa lakini sikuona haja ya kuondoka ni bora nifie hapa lakini leo hadi nionane naye.
“Nimegundua Diamond hana makosa. Mimi ndiyo kuna maeneo nilikuwa siko sahihi. Mama yake tulishamaliza tofauti zetu, tuko vizuri na ndiyo maana nikaona nimsake Diamond kwa udi na uvumba.”
AAMBULIA PATUPU
Licha ya kushinda kwa matumaini studio hapo hadi jioni, Risasi Jumamosi lilimshuhudia mzazi huyo akiondoka bila mafanikio kwani licha ya wasanii wa Diamond kudaiwa huwa wanafanya mazoezi karibu kila siku kwenye nyumba hiyo, siku hiyo geti halikufunguliwa hadi mzazi huyo alipokata tamaa na kuamua kuondoka zake.
DIAMOND HAPATIKANI
Gazeti hili lilifanya juhudi za kuwasiliana na Diamond kuhusu suala hilo lakini halikuweza kupata mawasiliano yake ya moja kwa moja baada ya marafiki zake kudai kuwa yupo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya shughuli zake za kimuziki.
TUMEFIKAJE HAPA?
Diamond na baba yake waliingia kwenye bifu zito baada ya mzazi huyo kumtuhumu mwanaye kuwa hamjali kwa sababu tu ana ugomvi na mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’.
Comments
comments