KWA kumwangalia tu kimwonekano hasa akiwa katilia mavazi yake ya kisanii, shati kubwa kama la kuvaa watu wanne, huku chini akipigilia suruali pana na viatu fulani hivi, lazima utavunjika mbavu.
Huyo ndiye Tajiri wa Kigoma a.k.a Brother K, msanii mahiri wa kuvunja mbavu anayetamba na kundi la vichekesho la Futuhi.
Ndiye anayetajwa kama mchekeshaji wa pili nchini kwa sasa anayependwa na kufuatiliwa kwa karibuni baada ya Mzee Majuto.
Staili yake ya kucheka na kuongea lafudhi ya watu wa Kigoma, imemfanya Brother K kuwa matawi ya juu, akiwapatia kinoma mashabiki wake na kile kitambi chake matata kinachochagizwa na mashati yake mapana.
Mwanaspoti limefanikiwa kumnasa na kupiga naye stori mbili tatu zilizozaa makala haya na amefunguka mambo kibao. Endelea.
ALIYEMSHAWISHI
Asikuambie mtu, baada ya King Majuto, Brother K ndiye anayefuata kwa kufuatiliwa na mashabiki wa vichekesho. Hata King Majuto amewahi kukiri, anakunwa na umahiri wa mvunja mbavu huyo akiamini ndiye mrithi wake. Brother K anajua kuchekesha bwana! Halazimishi kama baadhi ya wachekeshaji wengine, hata hivyo, hakuna anayejua alipotokea ama alivutiwa na nini hata kujitosa kwenye fani hiyo.
Brother K anakiri aliingia kwenye fani hiyo kama utani tu mwaka 2009, kutokana na ushawishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Videa Youth Center, Babu Pascal kukitambua kipaji chake na kumshawishi kuchekesha.
“Huyu ndiye aliyenifanya niingie kwenye uchekeshaji, kwani alikuwa akinisumbua kwa simu akitaka kujiunga na shirika lao ili kuendeleza kipaji nilichokuwa nacho.”
Anasema, licha ya maara kadhaa kumpiga chenga hatimaye aliamua kwenda kumsikiliza Pascal aliyekuwa akimtia moyo anajua kuigiza na kuchekesha na katu hapaswi kupuuza kipaji chake.
KUMBE ANACHANA BWANA!
Kama unadhani Brothe K ni mchekeshaji tu, umekosea. Jamaa alianza kutesa kwenye fani ya sanaa tangu mwanzoni mwa mwaka 2000 akiwa kama mwimbaji wa Bongo Fleva.
Anasema alikuwa mwimbaji wa kundi la Young Niger, lililokuwa likiongozwa na Baba Levo lililokuwa na maskani yake mjini Kigoma.
Mchekeshaji huyo anasema katika kundi hilo lililodumu kwa miaka miwili lilikuwa na wasanii wengine kama Christopher Charles, Fidel Ngeleja na Claudio Ntagunama ambao walifanya kazi nyingi na kujenga urafiki wa kudumu.
“Mbali na kazi ya muziki na jamaa hao, pia walikuwa marafiki zangu, kwani tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Majengo kule Kigoma na kazi zetu zilibamba sana.”
Anasema kundi lao halikudumu kwa vile kila mmmoja alikuwa na mishemishe za kusaka maisha na lilipovunjika, yeye na Carles maarufu kama Kijukuu walienda pamoja kujiunga na kundi la OBD mwaka 2006 na kudumu nalo kwa mwaka mmoja.
Anasema hata hivyo baada ya kuona wanafanya kazi bila kujitangaza na kuonekana wakaona bora wafanye mambo mengine, ndipo mwaka 2009 alipoonwa na Pascal na kumwingiza kwenye uigizaji na uchekeshaji kupitia Videa Youth Centre, lililokuwa huko huko kwao Kigoma.
Kituo hicho kilikuwa kikijishughulisha na sanaa ya maigizo, muziki, soka na vichekesho na ndipo alipoanza kung’arisha nyota yake baada ya ushawishi wa muda mrefu wa kujiunga nacho
DILI NJE NJE
Anasema kutokana na kituo chao cha Videa kuhusisha mambo mengi, kwa bahati yeye alimudu yote.
“Kulikuwa na michezo mingi sana, hivyo nikawa nacheza soka, kuigiza na kuchekesha, watu wakanipenda kwa uchekeshaji wangu, kwani kila aliyekuwa karibu yangu alikuwa akicheka kwani nilikuwa kama Mr Bean.”
Anasema kutokana na umahiri wake kulifanya dili zianze kumiminika kwake, baada ya Shirika la Ishi Kampeni kumchukua kufanya kazi ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.
“Mwaka 2010 nikapata kazi Shirika la Msalaba Mwekundu, tena wakati huo nakumbuka nilikuwa nasoma Chuo cha Ufundi Veta. Nilikuwa nasomea umeme wa nyumbani, lakini sikuishiwa vimbwanga.” Anasema aliifanya kazi yake kwa ufanisi huku akiendelea na masomo akiwa amebatizwa jina la utani la Kolo na pia akiwa kiongozi wa nidhamu.
SAFARI YA FUTUHI
Kama sio Futuhi, hakuna ambaye angekuwa akimfahamu Brother K, kwani kundi hilo ndilo lililomtangaza ndani na nje ya nchi, lakini alijiungaje?
Msanii huyo mwenye kiriba tumbo, anasema alijiunga na kundi hilo mwaka 2011 baada ya wafanyakazi wa RFA na Star TV, Paul Mabuga na Ahmed Baragaza kufika kituo cha Videa Youth Centre wakisaka wasanii wa kufanya nao kazi. Anasema watu wengi walijitokeza, naye hakuwa mmoja wao kwani siku watangazaji hao walipofika kituoni hapo hakuwepo.
Hata hivyo, walielezwa na mkurugenzi wa kituo hicho kuna mtu mmoja atawafaa na huku akimtaka (Brother K) akajiandikishe kujaribu bahati yake, japo alikuwa anakwepa mpango wake wa kutaka kujiunga na kundi hilo.
“Mimi nilikuwa nampiga chenga kama siku tatu hivi mfululizo, kila akinipigia simu ananiambia kwenda kusailiwa nikawa nakwepa.”
“Baada ya siku kadhaa nikaenda kwa Mabuga aliyekuwa anaandikisha majina, nilipofika akaniambia muda umeshaisha na sasa hivi tumebakisha majina matano ambayo tunataka kuyachuja ili wabaki wawili,” anasema Brother K.
Anasema kwa majibu hayo aliyafurahia kwani hata hivyo hakuwa na mzuka nao, akihisi ni kumpotezea muda tu na hakuna la maana kwenye usanii.
“Sikuhuzunika kwa kuwa ukweli sikuwa naota kuja kuwa mwigizaji au mchekeshaji, akili zangu zilikuwa kwenye muziki. Hivyo niliona poa, nikasepa zangu,” anasema.
BABU WA LOLIONDO AMBEBA
Hata hivyo, anasema siku chache akiwa hana hili wala lile, alipigiwa simu na kuambiwa aende kufanya usaili wa wazi mbele ya watu, ili ajumuishwe na wasanii watano walikuwa wamepenya kwenye mchujo.
Anasema siku hiyo ya usaili aliambiwa anatakiwa kuwachekesha watu waliohudhuria kushuhudia usaili huo. “Pale pale nilifikiria kitu cha kuwavunja mbavu watu hao ndipo akabuni mkasa wa Babu wa Loliondo, yule Babu aliyetamba na kikombe cha uponyaji, aisee kama utani watu walivunjika mbavu na kujikuta nikichukuliwa Futuhi.”
“Nilisimulia tu kisa cha Babu wa Loliondo, aliyekuwa akiwanyishwa watu kikombe cha dawa kwa Sh500. Akidai anatibu magonjwa mbalimbali ukiwamo Ukiwmi. Watu wote pale waliangua kicheko na kugalagala chini, basi nikaambiwa nitapigiwa simu na hapo ndio ikawa mwanzo wa kutua Futuhi,” anasema.
Unadhani siku yake ya kwanza kutua jijini Mwanza kuanza kazi na Futuhi, nini kilitokea? Je wazazi wake walikubali kumuacha aondoke Kigoma na yale mashati yake makubwa huwa anayatapata wapi? Ungana naye kesho Jumatatu.
By SADDAM SADICK, Mwanaspoti
Comments
comments