MOJA ya mradi uliopokelewa vizuri na mashabiki kwenye tasnia ya Bongo Fleva ni ule wa Dada Hood uliotayarishwa na mtangazaji wa XXL ya Clouds FM, Mamy Baby kwa ushirikiano na studio za The Industry.
Dada Hood ni project iliyowakutanisha marapa sita wa kike wanaofanya vizuri kwenye muziki wa Bongo Fleva kama vile Cindy Rulz, Pink, Chemical, Rosa Ree, Tammy na Stosh.
Kama hukupata bahati ya kuusikiliza wimbo huo unaweza kuvuta picha ya kitu gani kitatokea pale wanapokutana marapa hao wa kike kwenye Bongo Fleva kutokana na nyadhifa walizonazo.
Ni chemistry ya hatari sana kwa wadada wenye uwezo kukutana pamoja nyuma ya kipaza sauti.
Cindy Rulz
Japo hajatoa kazi mpya tangu mwaka 2013, Cindy Rulz ni miongoni mwa wasanii wachache wa rap walioweza kusikika nje ya mipaka ya Afrika na amekuwa msanii wa pili Tanzania kuingiza mashairi ya wimbo wake wa Lets Wait aliomshirikisha Dunga katika tovuti ya Rapgenius.com huko Marekani.
Pink
Umri wake mdogo haufanani na makubwa anayoyafanya pale akipewa nafasi ya kuchana. Pink maarufu kama Stylish Rapper, hivi karibuni amekuwa akigonga vichwa vya habari za burudani kutokana na ngoma yake Unafeel Aje kufanya vizuri kwenye redio na runinga nchini.
Ndani ya mradi wa Dada Hood, Pink alifanya yake na kuendelea kujijengea jina kwenye muziki wa Bongo Fleva. Kazi zake nyingine ni Usiogope aliofanya na Young Dee na Ngoma.
Tammy
Marehemu Albert Mangwea aliwahi kumtabiria makubwa rapa huyu na akamtunuku jina la Tammy The Baddest analolitumia mpaka hivi sasa.
Baada ya kushiriki kuweka mashahiri na sauti yake kwenye mradi wa Dada Hood, Tammy ameendelea kufanya poa kwenye vituo vya redio na runinga kwa ngoma zake kali ikiwemo hii mpya, Mtoto wa Kike inayokita kwa sasa.
Chemical
Amefanikiwa kuingiza ngoma zake kwenye chati mbalimbali za muziki ndani na nje ya nchi tangu miaka miwili iliyopita alipoachia kazi yake ya kwanza, Sielewi.
Anafahamika utunzi wake mzuri wa mashahiri ya rap yaliyojaa ujumbe, tambo na nakshi zinazoongeza ubora wake kwenye muziki wa Hip Hop. Sikiliza wimbo kama Forever, Kama Ipo Ipo Tu na Am Sorry Mama na Mary Mary.
Roza ree
Ni msanii anayemilikiwa na lebo ya The Industry chini ya Navy Kenzo. Roza Ree ni rapa wa kisasa mwenye uwezo kiuandishi na sauti yenye mamlaka pale anapochana.
Unaweza kuona uwezo wake ukisikiliza vesi ya kwanza ya mradi wa Dada Hood, kwenye wimbo wa Holla Holla, Up In The Air, On Time aliofanya na rapa Khaligraph Jones.
Kwa muda mfupi amefanikiwa kuwa balozi wa kinywaji cha Luc Belaire ambacho pia kinatangazwa na Rick Ross.
Stosh
Kupitia ngoma zake kama Walete aliomshirikisha Mr Blue na Waonyeshe zimefanya ajizolee mashabiki wengi wa muziki wa Hip Hop nchini.
Marapa hawa sita walikuwa kiungo muhimu kwenye mradi ule wa Dada Hood, sehemu ambayo ilikuwa ni jukwaa kwa wasanii wa kike kuonyesha vipaji kwa faida yao hasa ukizingatia kuna idadi ndogo ya wasanii wa kike kwenye Bongo Fleva.
Ukiwaangalia wote waliofanikisha mradi huo wa Dada Hood ni wadogo kiumri lakini wana uwezo na mtazamo chanya kwenye muziki wao.
Bado tunahitaji kazi zaidi kutoka Dada Hood zitakazoendelea kusimamia malengo ya mradi huo ulioandaliwa na mtangazaji Mamy Baby na studio za The Industry.
Na CHRISTOPHER MSEKENA
Comments
comments