Dakika 10 na Idris Sultan
Idris ambaye ni mchangamfu na mchekeshaji ukiwa naye, amefunguka mengi kuhusu maisha yake.
Mazungumzo yake ya dakika 10 na Starehe, ameelezea kuhusu uhusiano wake na Miss Tanzania 2006 Wema Sepetu kwa sasa, na skendo za mapenzi alizowahi kuhusishwa na baadhi ya mastaa akiwemo Linah Sanga.
Ukiwa na msongo wa mawazo ni kitu gani hufanya kukuweka sawa?
Sikimbilii pombe kwani kwa kufanya hivyo nitasahau kwa muda mfupi na baadaye nitakumbuka, sana sana nitakwenda kufanya kitu ambacho hunisahaulisha kabisa kama kuangalia filamu, nitaingia jikoni nitapika, naweza kwenda kusingwa ‘massage’, lakini moja ambayo huwa naifanya kuliko zote ni kuendesha gari usiku, ukisikia gari limepita kasi saa nane usiku ujue ni mimi.
Umewahi kutumia ustaa wako kuwarubuni wanawake na kutokana na umaarufu wako nini unakikosa?
Najiheshimu sana kwa sababu mimi ni msanii katika kitu ambacho siwezi kufanya ni kurubuni msichana, ukiona Idris anakufuata na kukutongoza ujue ni kweli amekupenda na anataka kuwa na wewe siko kama vijana wengine nipate ninachojisikia niondoke. Pili, siwezi kutoka na shabiki wangu hata siku moja, nawaheshimu wanawake ila naweza kuwa na uhusiano na mtu ambaye ni shabiki wangu lakini siyo kutoka naye kimapenzi.
Kuhusu umaarufu aisee wasichana nikiwafuata wananichukulia poa, wananiona kama sipo serious vile. Kwa kuwa ni mchekeshaji wanaona kama nawatania, kiukweli nawakosa (anaangua kicheko).
Vipi kuhusu Wema Sepetu?
Tuna zaidi ya mwaka mmoja sasa hatuko pamoja kwani hamjaona amewahi kusema anatoka na wengine (kicheko), tuko fresh tunaongea, lakini mpaka sasa sijui kama ninaweza kumwita rafiki lakini ndiyo hivyo tena.
Karibu wapenzi wangu wote wa zamani naongea nao, mimi ni mtu ambaye ukiachana na mimi ninajisikia vizuri kukupigia na tukazungumza, sina kinyongo kama nikiweka sababu kwa jinsi nilivyo basi ningekuwa na maadui wengi sana wanawake (kicheko).
Kwa nini tangu uachane na Wema hujawahi kuonyesha mwanamke mwingine hadharani?
Unajua nilikuja kugundua kwamba watu wengi wanafuatilia zaidi masuala ya mapenzi kuliko kile unachokifanya kwa wakati huo, nikaamua kuhamisha hisia zao kwamba kazi yangu kwanza na sitaki kazi yangu ibebwe na mapenzi. Hivi sasa najulikana kama mchekeshaji na shughuli zangu zingine zinaenda poa, hicho kitu kimenifunza sana.
Utakapotaka kuoa ni mwanamke wa aina gani utachagua?
Hahahaaa! Nipo makini sana katika hilo yaani acha kabisa. Kwanza lazima niangalie mwanamke mzuri na mwenye akili, masuala ya tabia na vitu vingine tutarekebishana. Sipo kabisa katika suala ya kuangalia tabia, maana naweza kumpata mwanamke ana tabia njema halafu huyu hapa (anaonyesha usawa wa magoti)mfupi balaa, huyu atanizalia watoto wa aina gani? Ninapofikiria neno ‘mke’ nafikiria pia atakuwa mama wa watoto wangu na nitapata watoto wa aina gani, kutengeneza watoto nayo ishu asikwambie mtu (anacheka).
Idris Sultan ni nani?
Alikuwa mpiga picha katika Kampuni iView Studio, umaarufu wake ulizidi alipojitokeza kushiriki mashindano ya Big Brother Africa – Hotshots mwaka 2014 na kushinda.
Idris aliyezaliwa Januari 28, 1993, ni mchekeshaji na mtangazaji katika kipindi cha MWB (Mji wa Burudani) katika redio ya Choice Fm.
By Herieth Makwetta, Mwananchi