RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika tasnia ya utengenezaji filamu na maigizo kutokana na mandhari na historia yake katika fani hiyo sambamba na mikakati liyojiwekea.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkongwe wa Filamu za Kihindi Kunal Kapoor aliyefuatana na Msimamizi wa Ofisi ya Utalii ya Zanzibar Mumbai, India Jilesh Babla ambapo mkongwe huyo yupo Zanzibar akiwa mgeni rasmi wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) mwaka huu.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeshachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho sheria inayohusiana na mambo ya filamu ili kuendana na Sera ambayo inasimamia tasnia hiyo.
Kutokana na hatua hizo Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inaweza kufanikiwa kuwa kituo cha uigizaji filamu kwa makampuni makubwa duniani ambayo yatakuja kutengeneza filamu zao jambo ambalo litaweza kuwainua wasanii wa filamu wa hapa nchini pamoja na kuinua pato la Taifa.
Aidha, Dk. Shein alieleza historia ya Zanzibar katika tasnia ya filamu na maigizo tokea mnamo miaka 1940 ambapo Zanzibar iliweza kutumika kama kituo cha uigizaji wa filamu mbali mbali kutoka kwa makampuni makubwa duniani pamoja na kuwa na majumba ya sinema na majukwaa na kumbi za maigizo hali ambayo Zanzibar inakusudia kuirejesha hivi sasa.
Kwa upande wa Ofisi ya Utalii ya Zanzibar iliyopo Mumbai nchini India, Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Ofisi hiyo katika kuitangaza Zanzibar na kupelekea kuongezeka kwa idadi ya Watalii kutoka India.
Dk. Shein alisema kuwa mafanikio zaidi yanaweza kupatikana baada ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Nae Mkongwe wa Filamu za Kihindi kutoka nchini India Kunal Kapoor, alieleza kuvutiwa kwake na mandhari pamoja na ukarimu wa Wazanzibari kwa wageni na hivyo kueleza haja kwa makampuni mbali mbali duniani kuja kutengeza filamu zao hapa Zanzibar zikiwemo Kampuni kutoka India.
Alisema kuwa katika kipindi kifupi alichofika Zanzibar ameweza kuona vipaji mbali mbali vya wasanii ambavyo iwapo vitaendelezwa na kukuzwa vinaweza kuendelea kuijengea sifa Zanzibar katika tasnia ya filamu na maigizo.
Pamoja na hayo, Mkongwe huyo wa Filamu za Kihindi na mtayarishaji mahiri na maarufu wa filamu kutoka Bollywood nchini India, alisema kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wake na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza tasnia hiyo ya filamu na maigizo hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa kutokana na uzoefu mkubwa alionao katika tasnia hiyo anamatumaini makubwa kuwa iwapo mashirikiano ya pamoja kati yake na Taasisi husika yataimarishwa Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa ikiwa ni pamoja na kujenga majukwa na kumbi za maigizo ya filamu za kisasa.
Sambamba na hayo, Kapoor ambaye ni mwongozaji na mtayarishaji wa filamu mashuhuri nchini India, alimuhakikishia Dk. Shein kuwa ana uwezo mkubwa wa kuyashajiisha makampuni kutoka nchini India kuja kutengeneza filamu zao hapa Zanzibar ikiwemo Kampuni ya Bollywood. “Uwezekano mkubwa upo wa kuzishawishi kampuni za India kuja kufanya filamu hapa Zanzibar kutokana na mandhari yake nzuri inayovutia”,alisema Kapoor.
Nae Msimamizi wa Ofisi ya Utalii ya Zanzibar iliyopo mjini Mumbai nchini India, Jilesh Babla alimueleza Dk. Shein mikakati iliyowekwa na Ofisi hiyo katika kuitangaza Zanzibar kiutalii pamoja na mafanikio ambayo imeshaanza kuyapata.
Kunal Kapoor ambaye anatoka katika familia ya waigizaji na watengeneza filamu maarufu nchini India, alikuwa mgeni rasmi katika Tamasha la ZIFF mwaka huu hapa Zanzibar ambalo hufanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na wageni mashuhuri, wasanii na wanamuziki na wadau mbali mbali wa kazi za sanaa duniani.
eatv.tv
Comments
comments