GODFREY Tumaini ndilo jina lake la kuzaliwa, lakini Bongo Fleva inamtambua zaidi kama Dudubaya, ingawa mwenyewe alijitahidi kwa kila hali kujiita Duduzuri bila mafanikio. Dudubaya ni mmoja kati ya ma-legend wa muziki huu wa Kizazi Kipya.
Ingawa naye aliwakuta watu ambao tayari walikuwa wameshaweka majina yao katika muziki huu, lakini bado yupo katika orodha ya wasanii wa mwanzo mwanzo walio-push kwa kiwango kikubwa Bongo Fleva.
Miaka ile ya mwanzoni mwa 2000, kwa tuliomfahamu angalau kwa karibu, jamaa hakufanana na alichokifanya jukwaani.
Akiwa na mwili mkubwa na mkakamavu, Dudubaya alikuwa kijana ambaye kama ungeambiwa ametoka kumpiga mtu sasa hivi, usingeshangaa. Lakini uliposikiliza tungo zake, hakufanana nazo kabisa.
Alipoamua kuimba mapenzi, aliyapatia kupita maelezo na hata alipotaka kuwapa mashabiki tungo zenye kusihi, kuonya na kufundisha, alifanya vizuri kabisa.
Jaribu kusikiliza nyimbo kama Mwanangu Huna Nidhamu, Nakupenda Mpenzi, Nimeondoka, Nakupenda Tu, Cheka Kidogo, Kiwango na Tingisha Kidogo utajua nini ninachomaanisha.
Dudu alifanya nyimbo kibao na nyingi zika-hit, kiasi kilichomfanya kuanzisha lebo yake ya Dar Skendo Halla, ambayo ilikuwa na wasanii kama Mac D na Dogo Hamidu ambaye sasa anajiita Nyandu Tozi. Kifupi ni kuwa Dudubaya ni staa mkubwa anayekaa levo moja na ma-legend wa Bongo Fleva unaowafahamu.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, Dudu ametoa kauli iliyomaanisha maoni yake juu ya Chid Benz, yule rapa mwenye uwezo mkubwa, anayejipoteza kwa kuendekeza ‘unga’ ambaye sasa yupo Rehab, Sober House, pale Bagamoyo.
Kwangu, maoni yake yalikuwa makali yaliyokaa kishari, kana kwamba ana ugomvi binafsi na Chid. Aliitaka jamii isimsaidie kijana yule wa Ilala kupata matibabu kwa sababu yeye mwenyewe hajijali, kwamba anatoa masharti kwa watu wanaotaka kumsaidia, achilia mbali kuwa ndugu zake hawaonekani kuwa mstari wa mbele kumsaidia.
Lakini kitu kibaya zaidi katika maoni yake ni ile kusema kwamba nchi yetu haina tatizo la ardhi, hivyo Chid Benz aachwe ajiue, atazikwa.
Ingawa ninamtambua Dudu kama mtu wa mavurugu, sikutegemea atoe kauli kama hii, hasa kwa kuzingatia kuwa Chid Benz ni mdogo wake, kimuziki na kiumri. Siku zote, mtu anayetoka nje ya mstari haachwi apotee, hushawishiwa kurejea!
Dudu mwenyewe ni shahidi wa jinsi gani watu walimvumilia kwa ile tabia yake ya kupenda kupigana ovyo na matusi yasiyochagua sehemu anapozungumza, wala nani anamzungumzia.
Leo vipi yeye anataka jamii imuache Chid Benz, kwa sababu tu hajirekebishi na ndugu zake hawaonekani? Pamoja na kwamba Chid ana ndugu, lakini familia yake kwa sasa ni muziki ambao mimi na Dudu ni wadau, hivyo ni jukumu letu kumsaidia, hata kwa mawazo, kama wengine tunavyofanya kupitia maandiko yetu.
Je, jamii ingeamua kumuacha yeye wakati ule, na pengine hadi sasa anapoendelea kuamini ngumi katika ulimwengu wa digitali, angekuwa vipi? Dudu my brother, tuungane kumpa sapoti mdogo wetu Chid Benz, anatuhitaji!
Chanzo:GPL
Comments
comments