Artists News in Tanzania

Familia Yakubali Barua Uchumba wa Wema, Manara

DAR ES SALAAM: Hivi karibuni, msemaji wa Klabu ya Simba ya jijini hapa, Haji Manara alisema anataka kumchumbia Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu akijipa matumaini kwamba hawezi kukataliwa, lakini habari mpya ni kwamba, mwanaume mmoja aliyedai ni mjomba wa Wema, ameongea na Amani na kusema kuwa, anamshangaa Manara.

Mjomba huyo alisema kuwa, anamshangaa Manara kwa kuwa ni mtu mwenye ufahamu na kwamba, ka   ma kweli anataka kumchumbia Wema, angeandika barua na kwenda kuipeleka nyumbani kwa mama Wema, Sinza Mori jijini hapa. “Sisi kama familia hatuwezi kukataa barua ya uchumba.

Tunaikubali kabisa lakini sasa kama kweli ana nia hiyo kwa nini asiandike na kutuletea nyumbani badala ya kusema kwenye vyombo vya habari? “Jamii tunayoishi, barua ya posa ya uchumba huwa haikataliwi, tutaipokea, tutaisoma na kumwita Wema mwenyewe kumuuliza atasema nini, labda kama Manara alikuwa akisema kwa utani maana alisema kuna sheria za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sijui zimefanyaje huko, zikipita sijui zisipopita angekuja kumposa Wema na kama akikataliwa angetembea bila nguo. Labda kama alisema utani,” alisema mwanafamilia huyo.

Baada ya madai hayo, Amani lilimtafuta Wema kwa njia ya simu ili kumuuliza aliichukuliaje kauli ya Manara lakini simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Akatumiwa ujumbe kwa njia ya Mtandao wa WhatsApp ambapo ilionesha wazi kwamba aliusoma lakini pia hakujibu.

Kwa kuona suala lenyewe limekaa kifamilia zaidi, ndipo juzi, Amani lilifika nyumbani kwa mama mzazi wa Wema, Mariam Sepetu ili kumsikia anasemaje kuhusu maneno ya Manara na maneno ya mtu aliyesema ni mjomba mtu kwamba familia inakubali kupokea barua ya uchumba.

Nje ya nyumba ya akina Wema, Amani lilipokelewa na mzee mmoja aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wa mama huyo na kukaribishwa kukaa kwenye viti baada ya kueleza shida.

Msaidizi huyo aliinuka na kwenda kupeleka ujumbe wa waandishi kwa mama Wema, baada ya muda alirudisha majibu kwamba, mama Wema hawezi kuzungumza na waandishi wa habari maana alikuwa na kazi zake za kufanya. Mwandishi: Tunaomba tuzungumze naye hata kwa njia ya simu. Msaidizi: Haiwezekani, nyie nendeni mtamtafuta wakati mwingine, yupo bize sana leo.

Mwandishi: Sawa lakini suala letu ni dogo sana, halichukui hata dakika moja kulitolea ufafanuzi, ni kweli hatukatai yupo bize, lakini hebu tusaidie pia hili, tukueleze kilichotuleta hapa, ukamuelezee akufafanulie, kisha uje utueleze.

Msaidizi: Hapana yote hayawezekani, nafikiri tumalizie hapa, nyie mnaweza kuondoka.

Alipomaliza kuzungumza maneno hayo, msaidizi huyo aliwataka waandishi kutoka nje ya geti jambo ambalo walitekeleza, lakini walipofika nje hawakuweza kuondoka mara moja waliendelea kukaa kumsubiri mama Wema atoke waweze kumdaka na kumfikishia ubuyu waliokuwa nao.

Kama walivyotegemea, baada ya nusu saa, mama Wema alitoka akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Harrier, waandishi walipomkimbilia alikanyaga mafuta na kuondoka zake huku akiwa amepandisha vioo vya gari ambavyo ni vya giza ‘tinted’.

Amani likampigia simu Manara na kumuuliza kuhusu kauli yake hiyo ya kutaka kumchumbia Wema ambapo alisema: “Nia iko palepale. Kuna wazee fulani nasubiri kukaa nao kuwaambia, baada ya hapo naandika barua na nitaipeleka kweli. Kwani nyie mnafikiri ni uongo? Hapana nitapeleka barua yangu ya uchumba kule!”

Chanzo: GPL

 

Comments

comments

Exit mobile version