Filamu Ya ‘Chungu Cha Tatu’ Yamalizika Sokoni , Wauza Feki Mbaroni
Kopi za filamu mpya ya JB na Wema Sepetu, ‘Chungu Cha Tatu’ zilizoingia sokoni Jumatatu hii zimemalizika ikiwa ni siku tatu toka iachiwe.
Akizungumza na Bongo5 Alhamis hii, JB alisema kasi ya mauzo ya filamu hiyo, ina kila dalili ya kuvunja rekodi ya filamu yake iliyopita Mzee wa Swagga.
“Filamu inaenda vizuri sana, Jumatatu baada ya kuingia sokoni masaa manne kopi zilizoingia sokoni ziliisha, Jumanne tukazalisha tena zikaisha, leo hii tumezalisha nyingine nyingi kwa sababu hata mikoani nilipigiwa simu kwamba zimeisha. Kwahiyo nashukuru mashabiki kwa kuonesha kuniunga mkono,” alisema JB.
JB alisema filamu hiyo imemgharimu takriban shilingi milioni 68 mpaka kukamilika.
Pia kwakusisitizia swala hilo, JB amefafanua zaidi kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa instagram hii leo.
“Kwanza nawashukuru sana sana kwa kuipokea vyema filamu ya Chungu cha tatu. …pili nawaomba radhi wote ambao jana walikosa nakala zao kwani iliisha tena…lakini leo ipo madukani baada ya mimi mwenyewe kukesha kiwandani nikihakikisha oda zote watu wanapata..mikoani pia sehemu ambazo ziliisha leo zipo…nimepata habari za watu wanaouza feki tayari baadhi yao wako ndani…asanteni..”