Filamu ya Hamisa Yatikisa Jiji
FILAMU ya mwanamitindo Hamisa Mobeto iliyozinduliwa wiki iliyopita, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Suncrest Cineplex uliopo ndani ya Quality Center, uliopo Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, hivi sasa inatikisa jiji kwa kile kinachotajwa kuwa ina kiwango kikubwa cha ubora.
Kwa mujibu wa wadau waliozungumza na Risasi Mchanganyiko juzikati, filamu hiyo iitwayo Zero Player, imechukuliwa kwa viwango bora kabisa kuliko kazi nyingi zilizotolewa siku za hivi karibuni na zaidi ya hapo, pia hata waigizaji wake waliifanya kwa ubora wa hali ya juu.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mwanamitindo huyo ambaye alicheza filamu hiyo na wasanii wengine kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Afrika Kusini, Ghana, Cameroon, Nigeria na Tanzania na pia filamu hiyo imerekodiwa katika kiwango kizuri sana na kila mmoja amecheza inavyopaswa katika nafasi yake.
“Kwa kweli ni filamu ambayo nimecheza lakini hata mimi mwenyewe naifurahia jinsi nilivyoitendea haki nafasi yangu, imenionyersha kiasi gani nimekua katika tasnia hii,” alisema Mobetto, mama wa watoto wawili. Baadhi ya wasanii walioudhuria uzinduzi huo walipongeza filamu hiyo na kusema kuwa imechezwa katika kiwango kizuri sana na chenye ubora wa uhakika huku wakiwapongeza wasanii ambao wamecheza filamu hiyo.
“ Yaani kiukweli nimeangalia filamu hii nimependa sana jinsi walivyocheza wameonekana wako makini na wanajua ni kitu gani wanakifanya katika uigizaji huo na pia wameweza kuwafunika hata wakongwe” alisema Ester Kiama
Chanzo:GPL