Artists News in Tanzania

Flaviana Matata: Mwanamitindo, Mjasiriamali na Mwanaharakati

Miaka 10 iliyopita Flaviana Matata aliibuka mshindi katika mashindano ya Miss Universe nchini. Huenda wengi walimchukulia kama washindi wengine ambao hufurahia umaarufu na zawadi kisha hupotea.

Miaka 10 baadaye Flaviana si tu jina maarufu nchini kama yalivyo mengine, ni super model, mjasiriamali na mwanaharakati anayesaidia wenye uhitaji.

Amefanyakazi na makampuni makubwa katika kazi yake ya uanamitindo na dili la hivi karibuni la kutangaza bidhaa za kampuni ya American Express ni mfano hai wa ukubwa wake katika biashara yake.

Wengi wanamtaja Flaviana kama mwanamitindo wa aina yake kuwahi kutokea katika nchi hii kwamba anaibeba nchi na kuitangaza vilivyo.

Ametoka mbali, lakini anasema anaendelea kujifunza na kupigania ndoto zake za kupanda katika majukwaa ya wabunifu nguli duniani– Alexander McQueen, Tory Burch na Vivienne Westwood.

Kwa hadhi yake anaweza kukutana na yeyote mfano, mzuri ni picha zinazomuonyesha akiwa na Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump.

“Ninakuwa mtu tofauti ninapokua kazini lakini baada ya hapo mke, dada na mtoto. Kaka zangu na baba wananikumbusha hivyo,” anasema Flaviana ambaye mama yake alifariki katika ajali ya meli ya MV Bukoba miaka 22 iliyopita.

Anasema miaka mitano ya mwanzo baada ya kushinda taji la Miss Universe ilikuwa ya kipindi cha mpito: “Nilikuwa najifunza mbinu za biashara ya mitindo. Nilianzia Afrika Kusini baadaye nikahamia New York Marekani.”

Kuhusu ndoa

Kwa wengi hasa walio katika biashara ya burudani ndoa inaweza kuwa kikwazo lakini kwa Flaviana ni tofauti na mwenyewe kwa neno moja tu anasema ni Baraka.

Anasema imekuwa chachu ya kuendelea kufanya vizuri kwani mume wake anamuunga mkono na kumsukuma kufanya kazi zaidi tofauti na awali.

“Kazi ya uanamitindo ina changamoto nyingi mwanamke asipopata mume anayeielewa biashara hii atakwama, anahitaji kuungwa mkono,” anasema.

Pamoja na kuwa ameolewa anasema bado anafuata miiko ya kazi yake na mume wake anamuunga mkono kwa kuwa anaelewa hiyo ni kazi yake.

“Nafanya kazi ya mitindo kama ajira, nina biashara ya rangi za kucha na mfuko wa kusaidia wenye uhitaji The Flaviana Matata Foundation (FMF), vyote hivi vinanihitaji.”

Kuhusu kuanzisha familia kwa maana ya kupata watoto anasema ni baraka na kwamba watakapokuja atawapokea kwa kuwa hawatakuwa kikwazo katika kazi zake.

“Siwezi kusema moja kwa moja ni lini lakini watoto ni baraka ambazo kila mmoja anafurahia kuzipata. Tofauti na watu wanavyofikiria wapo watu ninaowafahamu wanafanya vizuri katika kazi pamoja na kuwa na watoto. Unapokuwa mjamzito au kulea unaweza kuendelea na kazi. Hata hapa ninapoongea si kwamba huwa nafanya mitindo ya kuonyesha mavazi jukwaani, nafanya mara chache sana,” anasema.

Kuhusu Lavy

Mwaka 2015 Flaviana alifungua ukurasa mwingine kwa kujiingiza rasmi katika ujasiriliamali kwa kuingiza sokoni rangi zake za kucha ziiitwazo Lavy.

Anasema mzigo wake wa kwanza kuuingiza nchini uliisha ndani ya wiki mbili: “Nilitamani kufanya biashara muda mrefu lakini niliogopa soko, nilijiuliza namna watu watakavyozipokea bidhaa zangu.”

Anasema kilichomwogopesha ni ukweli kwamba watu wengi nchini huichagua bidhaa kutokana na bei yake na si ubora.

Anaongeza: “Nilitaka kutengeneza kitu tofauti. Nilichukua muda kutengeneza rangi ambayo inaweza kutumiwa na kila mtu kuanzia mama mjamzito mpaka mtoto.”

Rangi hizo zimepokelewa vizuri katika soko: “Zinapendwa na kununuliwa sana, kwa hilo namshukuru Mungu na watu wote wanaoniunga mkono.”

Trump na Russell

Kipara na nywele fupi ndizo zinazomtambulisha katika ulimwengu wa mitindo na kwamba hana mpango wa kuubadili mtindo huo kwa sasa.

Kupata dili za kufanya kazi na kampuni kubwa kumemfanya ajikute akiwa karibu na watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa duniani.

Anasema alikutana na Donald Trump kabla hajawa Rais wa Marekani: “Ni mtu anayependa watu wake pamoja na kuzungukwa na watu wengi lakini anakumbuka majina ya kila mmoja.”

Kuhusu Russell Simmons ambaye amewahi kuwa mume wa mwanamitindo Kimora Lee, anasema wamekuwa ndugu kutokana ukaribu walionao.

Kuhusu FMF

Mbali na kazi anapenda kusaidia wenye uhitaji. Katika kipindi kifupi alichofanya kazi Marekani alirudi nyumbani kuanzisha taasisi ya kusaidia wasichana nchini ya Flaviana Matata Foundation.

“Hii ndiyo namna pekee ya kuwasaidia wenye uhitaji, hata kama ni wasichana 20 tu basi ninahakikisha wanakaa darasani wakipata mahitaji yote muhimu ya shule,” anasema.

Anasema wasichana ndio taa ya Taifa lolote ndio maana anawahimiza kuweka bidii katika masomo yao.

Mwananchi

Comments

comments

Exit mobile version