Flora Mbasha Achumbiwa, Kuolewa Tena
Dar es Salaam. Baada ya wanandoa ambao ni wanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili, kuingia katika mzozo miaka minne iliyopita, mmoja wao Flora Mbasha amechumbiwa na anatarajiwa kufunga ndoa ya pili hivi karibuni mkoani Mwanza.
Sakata hilo linaweza kuibua mjadala miongoni mwa waumini wa dini ya Kikristo ambayo pamoja na kuruhusu ndoa kuvunjika, ni nadra sana kwa makanisa kuidhinisha suala hilo.
Habari za kuaminika ambazo Mananchi Digital imezipata zinasema vikao vya maandalizi ya harusi hiyo vimeshaanza baada ya Flora kufanikiwa kupata talaka aliyoidai Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini hapa.
Flora, ambaye ni mjukuu wa aliyekuwa muhubiri maarufu nchini, Askofu, Moses Kulola (sasa marehemu), tayari amevishwa pete ya uchumba na amebadili jina la kisanii akitaka mashabiki wake wamtambue kama “Madame Flora” badala ya jina aliloibukia la Flora Mbasha.
Asili ya neno “madame” analotumia Flora ni Ufaransa na linamaanisha mwanamke aliyeolewa.
“Kwa sasa siwezi kukwambia chochote kuhusu hilo. Sijui, labda ifikapo Machi naweza kuzungumza,” amesema Flora, ambaye alitamba na kibao cha “Jipe Moyo”.