Huyu Ndiye Gigy Money Mpya
ALITOKA kwa staili ya peke yake. Akapewa majina yote. Pengine majina hayo alistahili kwa namna alivyojiweka na kujitangaza mbele ya jamii.
Isingekuwa rahisi kumtabiria makubwa, ungeweza kuishia kusema ni msichana wa mjini, mwenye mambo mengi yasiyo na staha. Asiye na uoga mbele ya jamii ya wastaarabu.
Wakati anaanza kujulikana kwenye ulimwengu wa burudani, alifahamika kama video vixen, aliyepamba video za wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva. Akawa maarufu kutokana na umbo lake matata na picha zake za mapozi ya kimahaba kwenye mitandao ya kijamii.
Ndiyo njia aliyojichagulia katika kutaka kuchomoka. Kila kukicha ikawa ni tukio baada ya tukio. Visa baada ya visa. Mitandao ya kijamii ikaanza kumpamba kwa kila anachokifanya.
Bahati mbaya mwenyewe hakuchagua maneno ya kuongea, kila alichoongea aliona sawa tu. Hakuwa na muda wa kuchagua jibu la kutoa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Namzungumzia Gigy Money ambaye jina lake halisi alilopewa na wazazi wake ni Gift Stanford. Gigy Money alijitahidi kujipenyeza ili ajulikane kwenye jamii, ni jambo alilolifanya kwa nguvu kubwa na kwa hakika kwa hilo alifanikiwa kwa asilimia zote.
Kuna stori nyingi kuhusu Gigy Money. Nikianza kuandika nafasi haitatosha – ana mengi. Mwenyewe amewahi kukaririwa kwa nyakati tofauti akidai kutoka na mastaa kibao wa Bongo wakiwemo Hemed PHD, Rich Mavoko’, Ali Kiba, Ney wa Mitego, Matonya na Ommy Dimpoz.
Baadaye akasema anatamani kutoka na Diamond Plantnumz lakini anaheshimu hisia za mwanamke mwenzake – Zari The Boss Lady, mpenzi wa Diamond. Alisema eti anataka kumalizana naye ili awe ametoka na wababe wote wa Bongo Fleva baada ya kutoka na Kiba.
Yapo matukio mengine mengi, lakini kifupi alikuwa mtu wa vurugu za mitandaoni akijihusisha zaidi na mambo ya mapenzi. Kali kuliko yote, alisema hajui idadi ya wanaume aliotoka nao!
Unaweza kuona ni msichana wa namna gani. Tuyaache hayo kama yalivyo na ninatamani sana kwa sasa tumzungumzie Gigy Money mpya ninayemuona.
Gigy Money ambaye pia ana kipaji cha utangazaji mwenye sauti ya kuvutia, kwa sasa anafanya vizuri kwenye muziki wa Bongo Fleva. Kati ya singo zake zinazofanya poa zaidi ni pamoja na Nampa Papa ambao ni moto wa kuotea mbali na unazidi kumpaisha.
Wakati anaanza muziki na kujitanabaisha kama mwanamuziki wa Bongo Fleva, wengi walimbeza, hata mimi sikuwa na imani naye sana kutokana na namna aliyojiweka awali, nikaamua kujipa muda.
Ni kweli baada ya kujipa muda, nimekuja kugundua kitu cha tofauti kabisa. Kwamba Gigy Money si wa mchemchezo kwenye muziki. Kitu pekee ninachotamani kitokee kwake ni kutorudi nyuma tena kwenye matope. Sasa asimame kwa miguu miwili akitetea kipaji chake cha muziki alichokionyesha.
NAMPA PAPA
Songi lake la Nampa Papa ndilo ambalo limeonekana kumpa shavu zaidi kiasi kwamba kila unapopigwa, mashabiki wa Bongo Fleva huguswa na wimbo huo.
Hata hivyo ana pini nyingine inayokwenda kwa jina la Supu, ambayo nayo ni kali lakini haifui dafu mbele ya Nampa Papa ambao ni gumzo kila kona na unapopigwa kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni.
SHOO ZA FIESTA
Ili kuelewa ukubwa wa Gigy Money kwenye Bongo Fleva, yeye amekuwa miongoni mwa wasanii waliopanda kwenye jukwaa hilo katika mikoa mbalimbali nchini mwaka huu.
Pengine tungeweza kusema waandaaji wa Fiesta wamempendelea kumpa shavu hilo lakini shangwe alilokuwa akilipata kila alipopanda kwenye jukwaa la Fiesta ni kielelezo tosha kuwa anao uwezo mkubwa kwenye Bongo Fleva.
Tunapozungumzia Fiesta kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva, tunazungumzia msimu mkubwa wa burudani, unaokusanya wasanii wenye ushawishi mkubwa – mastaa na chipukizi katika jukwaa moja.
Gigy Money kupanda kwenye jukwaa hilo na kushangiliwa na mashabiki ni alama tosha kuwa viatu vya muziki wa Bongo Fleva vimemtosha.
MBELE KWA MBELE
Kwa sasa Gigy Money anatakiwa kuachana na yaliyopita. Ameingia kwenye ngoma yake. Acheze tu sasa. Anaweza kufanya makubwa na kuishangaza dunia kwenye muziki. Cha kujivunia zaidi ni kwamba ana umbo na sura nzuri isiyochosha kutazamwa na mashabiki jukwaani.
Uzuri wa sura na umbo lake avitumie jukwaani akisindikiza na kipaji chake cha muziki ambacho awali kilifichwa na matukio yake ya social media.
GIGY MONEY: SIRUDI NYUMA
Gigy Money mwenyewe amekiri kwamba yote yaliyotokea ni katika kutafuta kutoka na kwamba kwa sasa hatarudi nyuma, badala yake atasonga mbele kuonyesha kipaji chake cha muziki.
Akizungumza juzi Alhamisi katika redio moja jijini Dar es Salaam, Gigy Money alisema: “Mimi najijua nina vipaji vingi, tatizo lilikuwa ni namna ya kutoka. Leo hii watu wanaelewa muziki wangu, mwanzo nani angenielewa?
“Ilikuwa lazima nipitie mapito yote hayo, maana wasanii wengi walikuwa wanabana, watu hawakutaka kunipa nafasi, nikachagua njia ya kuwa Gigy Money… watu wanijue kwanza, nashukuru hilo nimefanikiwa.
“Kwa sasa nafanya muziki na ninashukuru umekubalika. Gigy wa sasa ni wa bei mbaya, hakuna mtu wa kunilipa kwenye video za wasanii, zamani ilikuwa sawa maana nilikuwa natafuta kutoka, sasa nipo vizuri nafanya muziki.”
Mtanzania