STAA wa filamu za Kibongo Irene Uwoya, ameendelea kugonga vichwa vya habari za burudani baada ya mume wake, Hamad Ndikumana aliyefunga naye ndoa ya Kikristo kufariki dunia mapema wiki hii akiwa nyumbani kwake, Kigali nchini Rwanda.
Kwa wiki tatu mfululizo Uwoya amekuwa hakuauki kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa tukio aliloliita ni ndoa ya Kiislamu aliyofunga na msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’, ndoa ambayo Janjaro alithibitisha siyo filamu, licha ya Uwoya kudai ni filamu.
Mfululizo wa tukio la ndoa mpya na msiba wa mume wake, Ndikumana yamepokewa kwa mitazamo tofauti na mashabiki wake. Wapo waliompa pole huku wengine wakimtusi.
Wanaomtusi wanahusisha tukio lake la ‘ndoa tata’ na Janjaro kuwa huenda limemuumiza Ndikumana kiasi cha kupata mshtuko wa moyo na kupoteza maisha. Hata hivyo, kwa jumla wengi wameonyesha kuguswa na msiba huo na kuonyesha hisia zao.
Katika kundi hilo ambalo lina watu wengi zaidi, wamekwenda mbali zaidi na kuumizwa kwa msiba huo kiasi cha kufananisha na pigo alilopata mzazi mwenzake na msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Zari The Boss Lady baada ya kufiwa na aliyekuwa mumewe Ivan Don.
NDOA
Uwoya aliolewa na kocha huyo msaidizi wa Klabu ya Rayon Sports ya Rwanda mwaka 2009 na katika maisha yao ya ndoa walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Krish, ambaye amekuwa akiishi naye jijini Dar es Salaam.
Upande wa Zari, naye alifunga ndoa ya kimila na mfanyabiashara wa Uganda, Ivan Ssemwanga ‘Ivan Don’ miaka mingi iliyopita na katika maisha yao ya ndoa walifanikiwa kupata watoto watatu wa kiume.
CHANGAMOTO NDANI YA NDOA
Mwezi uliopita, Uwoya na mzazi mwezake marehemu Ndikumana, walianza kutupiana maneno kwenye mitandao ya kijamii ambapo Ndikumana alitoa malalamiko kwa mrembo huyo kuwa katika maisha yao hakuwa mkweli ikiwa ni pamoja na kumnyima haki ya kumsalimia mtoto wao, Krish anayeishi Bongo na yeye akiwa anaishi Rwanda.
Malalamiko hayo, Uwoya aliyakanusha na zaidi aliendelea kufanya mitikasi yake ikiwa ni pamoja na kula bata nchini China hata aliporejea nchini, Octoba 27, mwaka huu akadai kufunga ndoa na Dogo Janja, jambo ambalo lilionekana kutomuumiza Ndikumana.
Alichofanya Ndikumana ni kujibu mashambulizi kwa kumtangaza mpenzi wake mpya wa Kinyarwanda, aliyemtaja kwa jina la Asmah na kuendelea na maisha yake ya furaha huku akionyesha kutokuwa na presha na ndoa ya Uwoya na Dogo Janja kwani mrithi wake aliweza kurudisha tabasamu lake lililopotea. Hiyo ilikuwa Oktoba 31, mwaka huu.
Upande wa Zari, raia huyo wa Uganda aliachana na mume wake Ivan Don mwaka 2014 baada ya kunasa kwa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambapo mpaka sasa wamepata watoto wawili, Tiffah na Nillan.
Zari alikuwa karibu mno na watoto wake aliozaa na Ivan Don licha ya vijana hao wa kiume kuishi na baba yao Uganda na Afrika Kusini lakini hakuwahi kuonyesha nia ya kumrudia mumewe zaidi ya kuboresha panzi lake jipya na Diamond Platnumz.
Ivan Don kwa muda wote huo akiwa mbali na mke wake alionyesha kuwapenda watoto wake, kusimamia miradi yake iliyopo Afrika Kusini na Uganda pamoja na kula bata na kundi lake la Rich Gang bila kuwa karibu na mrembo mwingine.
VIFO VYA WAUME ZAO
Kifo cha Ndikumana kimetokea ghafla usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki hii, akiwa nyumbani kwake. Inadaiwa alipata tatizo la maumivu ya kifua kabla ya mauti kumkuta.
Siku nzima kabla ya kifo chake alikuwa mzima, hata jioni yake alikuwa mazoezini akiwanoa wachezaji na yeye mwenyewe akishiriki mazoezi.
Afisa Habari wa klabu hiyo aitwaye Gwakaya alisema Ndikumana alipata maumivu makali ya kifua na akaomba soda ya baridi, alipomaliza kunywa kidogo akatapika kisha akakata kauli hivyo anadhaniwa amekufa kwa ugonjwa wa moyo.
Ndikumana ni baba wa watoto wawili wa kiume Baasit na Krish. Alizikwa Jumatano kwenye mjini Nyamirambo, Rwanda.
Kifo cha Ivan Don, kilikuja baada ya tajiri huyo kuugua na Zari kushiriki katika kumuuguza kwenye Hospitali ya Stive Biko Academy, Afrika Kusini mpaka alipofariki kwa ugonjwa wa mshtuko wa moyo, Mei 25, mwaka huu na kuzikwa Nakarilo, Uganda.
UWOYA AVISHWA VIATU VYA ZARI
Kama unavyoona hapo juu, matukio yaliyotokea kwenye maisha ya Zari yanawiana kidogo na yale yaliyomtokea Irene Uwoya kwa kuwa wote waume zao wamepoteza maisha baada ya ndoa zao kuvunjika.
Mungu ailaze roho ya marehemu Hamad Ndikumana mahali pema peponi – Amina.
Mtanzania
Comments
comments