Hatimaye filamu ya kwanza ya aina yake inayohusisha joka kubwa linalosumbua wanakijiji na kumeza watu imekamilika kutengenezwa. Filamu hiyo iliyopewa jina la JOKA LA KIJIJI imetengenezwa na kampuni mpya ya Zakwetu Network.
Mtunzi na muongozaji wa filamu hiyo, Mkongwe Sultan Tamba ambaye ndiye aliyesukuma gurudumu la tasnia ya mlipuko wa filamu kwa kutunga na kutayarisha filamu maarufu ya Girlfriend.
Amesema hayo ni mapinduzi mengine ambayo tasnia inapaswa kujivunia kwa sasa kutokana na kutengenezwa katika kiwango cha teknolojia ya kisasa.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi, Tamba amesema ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kufanya filamu ya aina nyingine, yenye mtazamo mwingine na ndipo wazo la kulishirikisha joka hilo kubwa lilipomjia na kulifanyia kazi. “Nilikuwa na hadithi hii kwa muda mrefu.
Wasichana wawili walioenda kisimani walikutana na balaa la kushtukiza kwa kumwona chatu mkubwa aliyekuwa akiishi kisimani kuwatokea na kumuua mmoja wapo kwa kummeza. Na si kumeza mtu tu, joka hilo linaingia kwenye nyumba ya ‘mbavu za mbwa’ na kutaka kuishi humo. Wazo hili nimeamua kulifanyia kazi sasa hivi na kazi imekwisha.” Alisema.
Filamu hiyo iliyohusisha waigizaji wenye vipaji vya hali ya juu akiwemo Madebe Lidai, imehusisha teknolojia ya VFX ambayo Tamba alifanikiwa kuisomea kwa muda mrefu.
“Hili si joka la Kibisa, au Joka la kukodi mahali, ni joka tofauti, na limefanya mambo makubwa ambayo ni miujiza kuona likifanya kwenye filamu zetu, labda nje. Ni kazi yangu ya kwanza mwaka huu ambayo najivunia sana kwa sababu imekamilika kwa kiwango nilichotaka. Kama watu wamezoea kuona Chatu kwenye filamu za nje, sasa watapata kwenye filamu yangu pia.”
Filamu ya Joka la Kijiji imehusisha simulizi ya kusisimua ya mwanamke ambaye alimuua mume wake miaka mingi iliyopita kwa tamaa ya mali na sasa mambo yameanza kuvurugika.
FC
Comments
comments