Artists News in Tanzania

Kutoka na Staa, Lazima Ujipange Aisee

USTAA gharama! Inaelezwa hivyo na ndiyo ukweli wenyewe ulivyo. Mastaa wenyewe hupata wakati mgumu kutokana na kulazimishwa namna ya kuishi na taito zao kwa jamii.

Pengine utakuta msanii fulani angependa kupanda daladala kwa nauli ya shilingi 400 kwa ruti moja, lakini kwa sababu ya kuogopa macho ya watu na kulinda ‘image’ yake inambidi akodi taksi ya shilingi 7000.

Si ajabu angependa kuingia kwenye kibanda cha mama lishe na kujipatia chakula cha bei poa lakini kutokana na hadhi yake anajikuta lazima aende sehemu yenye hadhi ambayo anaweza kulipia chakula kwa bei ya mara kumi zaidi ya ile ya mama lishe.

Kazi ipo kwa mastaa wa kike ambao maisha yao huwa ghali zaidi kuliko wanaume, maana wao (wanaume) wanaweza kujitoa fahamu hata kwa kupanda daladala au kula chipsi mayai kwenye vibanda vya chipsi mitaani.

Ukiacha hayo yote pembeni, wapo baadhi ya wanaume wanatamani kuwa karibu na mastaa, pengine kwa urafiki tu au hata kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, lakini wanakuwa na hofu ya fedha maana wanajua wao ni matawi ya juu.

Hawajakosea ndiyo maana mastaa wengi wa kike ama wanaingia kwenye uhusiano na mastaa wenzao au mapedeshee wenye fedha zao.

Lakini kuna wale ambao wanatamani hata kutoka na staa mmoja wa kike na kukaa naye mahali fulani kwa chakula cha jioni. Hapo kidogo roho itasuuzika.

Mwandishi wa Juma3tata alifanya mahojiano na baadhi ya mastaa Bongo ili kujua gharama zao za kawaida kwa mtoko mmoja wa usiku, pengine kama kuna mtu ana ndoto ya kutoka naye.

Swali letu kwa mastaa hao lilikuwa: “Ikitokea mtu akataka kukutoa out jioni, kwa namna unavyojifahamu kwa hadhi yako, anatakiwa kujipanga kwa fedha kiasi gani?” Majibu yao ni kama ifuatavyo.

GIGY MONEY

“Mimi bwana siingii vihoteli uchwara, sehemu zangu za kula raha zipo Masaki na Posta, huko ndiyo kuna viwanja ambavyo Gigy anaweza kukaa na kupata chakula cha usiku kwa raha.

“Pande hizo lazima uwe vizuri, angalau mtu akiwa na 700,000 au 800,000 basi outing yetu inaweza kuwa nzuri. Hiyo ni kwa sababu kwanza nikiingia hotelini jioni cha kwanza ni package ya bia ndiyo masuala ya msosi tena wa nguvu yafanyike.”

AUNTI LULU

Msanii wa filamu Bongo aliyeibukia kwenye utangazaji, Lulu Mathias Semagongo ‘Anti Lulu’ yeye amesema shilingi 1,000,000 inaweza kuteketea bila huruma kwa mlo mmoja wa jioni hotelini.

“Milioni lazima ikate, tena napenda sehemu zenye fukwe nzuri na zilizotulia. Kifupi napenda sehemu za maficho, zisizo na macho ya watu. Pesa hiyo sijaweka gharama ya mafuta ya gari.”

DAYNA NYANGE

Msanii wa Bongo Fleva, Dayna Nyange yeye anasema shilingi 150,000 inatosha kwa mtoko mmoja wa jioni moja. Kiasi hicho cha fedha kinajumuisha gharama za chakula na vinywaji.

“Unaweza kuona ni pesa ndogo, lakini kwangu inatosha maana huwa situmii vinywaji vyenye vilevi. Sehemu zangu ninazopenda zaidi ni Lamada Hotel, Sea Cliff Hotel na White Sand au hoteli yoyote iliyopo ufukweni,” anasema.

SHAMSA FORD

Staa wa filamu za Kibongo, Shamsa Ford amesema yeye gharama yake ni shilingi 500,000 kwa mtoko wa jioni moja.

“Kwa kawaida mimi huwa napenda kuangalia menu kwanza, lakini napendelea zaidi kula chakula special cha siku ambacho kimeandaliwa na hoteli. Laki tano inatosha kabisa,” anasema.

ESTAR KIAMA

“Mimi ni staa hivyo huwa napenda kwenda sehemu za kistaa, kwa uchache pamoja na usafiri shilingi 200,000 au 300,000 inatosha kabisa. Kwa kawaida mimi huwa sihitaji vitu vya gharama sana, labda nikiwa na kampani yangu mara nyingi huwa natumia hadi shilingi 500,000, kwa hiyo mtu anayetaka kunitoa aandae pesa hiyo.”

Mtanzania

Comments

comments

Exit mobile version