Lady Jaydee Avunja Ukimya
Mkongwe wa muziki wa bongo fleva Lady Jaydee ametangaza rasmi kurudi tena kwenye muziki baada ya ukimya wa muda kidogo kwenye muziki. Lady Jaydee ameweka wazi ujio wake mpya kwenye muziki baada ya siku 30 kuanzia leo.
Wiki kadhaa zilizopita Lady Jaydee aliwahi kuwaomba wapenzi wa muziki wake kuwa wavumilivu na kuwataka wasubiri kwani kwa kipindi hicho alikiri wazi kuwa hana kitu cha kuimba wala hakuwa na mizuka ya kuimba, kutokana na mambo yake ya hapa na pale na kuwataka wapenzi wake kwenye muziki kudumisha amani.
“Karibu tu lakini sina lolote kwa sasa, sina kabisa na sitakuwa nalo kwa kipindi kirefu sana, yaani sina, sina, sina. wapenzi huvuta subira mashabiki huhama hama. Wapenzi vuteni subira na dumisheni amani” Aliandika Lady Jaydee
Baada ya ukimya na mashabiki kuanza kuhoji juu ya ukimya wake kwenye muziki, mwanadada Lady Jaydee alikuja na kuweka wazi kuwa amekuwa kimya lakini hawezi kufanya lolote sababu hakuwa na jambo la kusema au kuimba kwa wakati huo na kuwataka tena mashabiki na wapenzi wa muziki wake kuwa wavumilivu.
“Ni kweli sijasema ,ni kweli nimekaa kimya lakini siwezi sema tu endapo sina cha kusema mnaweza kuvumilia? Kama ninavyo vumilia? Napumzika tu sina cha kufanya mvumilie nitarudi sema sina cha kusema na siko tayari kusema, nitasema nikiwa tayari kusema” Alimaliza Lady Jaydee
Lady Jaydee sasa amepata cha kusema na amepata ya kuzungumza na ndio maana ametangaza rasmi ujio wake mpya kwenye muziki wa bongo fleva, Jide amesema kuwa baada ya siku 30 kuanzia leo atasimama tena.
Eatv.tv