-->

Lameck Ditto: Siyo Vizuri Kutangaza Mabaya ya Chid Benz

UKITAJA orodha wasanii wa Bongo wenye hadhi ya kuwa wanamuziki basi jina la Dotto Bwakeya ‘Lameck Ditto’ ni lazima liwemo. Mwimbaji huyu wa Moyo Sukuma Damu amekamilika kila idara yaani mbali na kuimba ni mtunzi na mpigaji wa ala za muziki.

Ni wasanii wachache sana Tanzania wenye uwezo wa kutumbuiza mubashara (live) kwenye jukwaa. Ditto anaweza kufanya hivyo, mashabiki wanaopenda muziki mzuri bila shaka watakuwa wamenielewa.

Juma3tata leo, tumepata nafasi ya kupiga stori mbili tatu na Lameck Ditto, alipotembelea ofisi za gazeti hili mwishoni mwa wiki ambapo amefunguka mambo kadha wa kadha yanayohusu maisha yake na tasnia nzima ya muziki hapa nchini. Karibu..

FAMILIA

Mashabiki wa muziki wamekuwa wakimfahamu, Lameck Ditto kupitia muziki, si rahisi sana kukuta akizungumzia mambo yanayohusu mapenzi yake binafsi kama wanavyofanya mastaa wengin, sababu gani inafanya awe hivyo?

“Familia yangu ipo vizuri kabisa ndiyo maana mimi nipo hapa, naishi na mzazi mwenzangu tuna mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minne,” anasema Ditto.

NAFASI YAKE THT

Ditto ni zao la nyumba ya vipaji, Tanzania House Of Talent (THT) na hapa anazungumza nafasi yake kwenye jumba hilo lililo nyuma ya mafanikio ya mastaa wengi wa Bongo Fleva.

“Mimi pale THT n mwanafamilia, ni kama nyumbani, muda wangu mwingi nautumia pale. Toka nilivyoingia miaka 7 iliyopita asilimia 75 ya siku yangu huwa naitumia pale, labla niwe na shoo au niwe kwenye mahojiano kama hivi leo nipo hapa kwenye gazeti la MTANZANIA,” anasema.

AMETUNGA NYIMBO ZIPI?

Kama nilivyosema hapo awali, Ditto amejaliwa kuwa ni vipaji vingi ikiwa ni pamoja na kutunga mashahiri ya muziki, Juma3tata lilitaka kujua mpaka sasa ametunga nyimbo zipi zilizobamba, mwenyewe anafunguka..

“Sina idadi kamili ya nyimbo ambazo nimetunga, kwa sababu kuna nyimbo nimetunga wameimba wasanii wengi, nimetunga nyimbo kama Miaka 50 ya Uhuru, Tuulinde Muungano Wetu na Ishi na Mimi ule ambao wasanii waliimba wakati Rais anazindua ujenzi wa bomba la mafuta kule Tanga, kwa upande wa wasanii nimeandika nyimbo kadhaa za Linah (Malkia wa Nguvu) na wengine,” anasema.

HALI YA CHID BENZ

Ikumbukwe kuwa Chid Benz ndiye aliyemuonyesha, Ditto, Jiji la Dar es salaam baada ya kumpokea na kukuza kipaji chake kwenye kundi la La Familia akiwa ametokea watu Pori chini ya Afande Sele kama hajajiunga na THT.

Lakini hivi karibuni rapa huyo anayefanya vyema na wimbo wake, Muda amekuwa akipita kwenye changamoto ambayo kila mmoja wetu anaifahamu ikiwa ni pamoja na kutangaza kufanya kolabo na JAY-Z, Je Lameck Ditto anaizungumzia vipi hali ya mlezi wake huyo?

“Mimi binafsi nimekutana na Chid Benz na kuongea naye, nikagundua ni mtu ambaye anatamani kutoka kwenye ile hali, kwa hiyo namna nzuri ya kumsaidia ni kumpa msaada kimya kimya, haina haja ya kumtangaza mabaya yake au kumwongelea vibaya, hiyo itamsaidia zaidi,” anasema.

SIRI YA KAZI YAKE MPYA

Baada ya kufanya vizuri na Moyo Sukuma Damu na Atabadilika hivi sasa anatamba na audio ya wimbo wake unaoitwa, Nabembea. Ipi ni mipango kazi yake kwa sasa baada ya kuachia ngoma hiyo?

“Huu ni wimbo wa kwanza kuandikiwa, nimekuwa nikiwaandikia sana nyimbo wasanii wenzangu, lakini huu ameniandikia dogo mmoja anaitwa Mario, aliuleta kwangu ukiwa umekamilika na ni mzuri, mimi nikauboresha ukawa hivyo ulivyo, video inatoka baada ya wiki moja kutoka sasa kwa hiyo mashabiki waendelee kuisapoti Nabembea,’ anasema Ditto.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364