Lulu Afungukia Kuhusu na Siasa na Wasanii
ELIZABETH Michael ‘Lulu’ amefunguka kuwa anajivunia uamuzi wake wa kutojihusisha na siasa maana amepata amani ya moyo kuliko wasanii wenzake ambao kwa sasa wapo kwenye malumbano ya kisiasa.
Mrembo huyo ambaye ni mkali wa sinema za Kibongo, alisema, wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu Mwaka 2015, watu wengi walikuwa walikuwa hawamuelewi lakini ukweli ni kwamba aliliona hili ambalo linatokea kwa sasa ambapo wasanii wanaumbuana, wanasemana na kuwagawa mashabiki.
“Unajua watu wengi walikuwa hawanielewi kwa nini sipendi siasa na ninajua wazi wengi waliniona labda mimi naringa sitaki kujumuika na wezangu lakini siyo hivyo nilijua nini kinaweza kutokea mbeleni kama ilivyo sasa,” alisema Lulu kufafanua anazungumzia malumbano yapi hasa.
Hivi karibuni, Muigizaji Wema Sepetu alitangaza kujitoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo alitupa dongo kwa CCM kwa kusema anawadai hela za kampeni hali ambayo iliwaibua wasanii wenzake, kumpinga vikali kwa maelezo kuwa walilipwa.