Artists News in Tanzania

Lulu Ashambuliwa kwa Maneno, Kisa Mama Kanumba

KITENDO cha muigizaji wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, kudaiwa kutoa maneno yenye kuonesha sawa na kumtusi mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa, baadhi ya watu wamesema kuna dalili za msichana huyo kuitafuta laana.

Hivi karibuni, mama Kanumba aliliambia gazeti moja nchini (siyo ya Global Publishers) kuwa tabia ya mpenzi huyo wa zamani wa mwanaye imebadilika sana na kukosa maadili, kiasi cha kumuita yeye kuwa ni kubwa jinga.

“Hata kama siyo mama yake mzazi, lakini umri tu unatosha kumuonesha kuwa anahitaji kumheshimu, huwezi kumuita mtu aliyekuzidi kubwa jinga, vinginevyo ni utovu mkubwa wa nidhamu na kwa mujibu wa mila na desturi za Watanzania, huku ni kama kutafuta laana, mama Kanumba ni kama mzazi wake,” alisema msomaji mmoja wa gazeti hili, aliyejitambulisha kwa jina la Tabia Doffa wa Kimara.

Msomaji mwingine aliyepiga simu chumba cha habari kutoka Tanga, aliyelitaja jina lake kama Aesha, alisema kinachoonekana umaarufu umempa upofu, kiasi cha kushindwa kuwaheshimu watu wanaomzidi umri, tena mtu ambaye angeweza kuwa mama mkwe wake, ikizingatiwa kuwa Lulu alikuwa mpenzi wa Kanumba.

“Huyu mtoto umaarufu umempoteza, huwezi kutoa maneno kama hayo kumwambia mtu ambaye angeweza kuwa mkweo, hivi kama Kanumba angekuwa hai angeweza kumwambia namna hiyo? Hili ni tatizo la malezi, mambo mengine ya ustaa ni ulimbukeni tu, laana inamnyemelea huyu,” alisema Aesha.

Akizungumzia suala hilo, mama Kanumba alisema anasikitishwa sana na tabia ya msichana huyo, kwani kikubwa ambacho angefarijika kupata toka kwake ni heshima tu na wala si kingine chochote.

“Sielewi jambo gani limemtokea huyo binti mpaka kufikia hatua ya kuniita hivyo, lakini yote namwachia Mungu maana anajua anachokifanya,” alisema mama huyo huku akionekana kulengwa na machozi.

Kwa upande wake, alipoulizwa kuhusu kutoa kauli nzito kwa mama huyo, Lulu alisema hapendi kumzungumzia chochote kwani siyo staili yake kuzungumzia mambo ya wengine katika vyombo vya habari.

“Kama yeye amesema hivyo kwenye vyombo vya habari ni staili yake, mimi staili yangu ni ya kukaa kimya, sitaki kabisa kumzungumzia huyo mama,” alisema Lulu.

Chanzo:GPL

Comments

comments

Exit mobile version