Artists News in Tanzania

Magufuli Ataka Kufuta Hati ya Shamba la Chavda

Rais John Magufuli amesema anasubiri taarifa kutoka kwa kamishna wa ardhi ili aweze kuifuta hati ya shamba la Chavda na kulirejesha kwa wananchi.

Rais John Magufuli

Amesema notisi ya ombi la kufuta shamba hilo tayari siku 90 zimemalizika hivyo inasubiri mchakato wa kamishna wa ardhi amuandikie barua.

Ametoa taarifa hiyo leo Alhamisi, Agosti 3 baada ya Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (Profesa Maji marefu) kulalamika kuwa mashamba ya mkonge hayaendelezwi huku wananchi wa jimbo lake wakikosa ardhi ya kilimo.

“Mheshimiwa Rais nakushukuru kwa kunipeleka India kutibiwa, lakini kero kubwa ya wananchi wa jimbo langu in uhaba wa ardhi…mashamba ya mkonge hayaendelezwi yamebakia pori tu naomba unisaidie wananchi wapewe,” amesema Maji Marefu.

Akizungumzia mashamba ya Mkonge, Rais Magufuli amesema tayari alishafuta hati za mashamba matano ya mkonge ya Wilaya ya Muheza yenye jumla ya hekta 14,000 na kuzirejesha kwa wananchi.

Amesema anasubiri kwa hamu barua ya kamishna wa ardhi ili aweze kufuta kulingana na mapendekezo kwani hakuna shamba lililowasilishwa kwake likapona kufutwa.

Rais Magufuli ambaye yupo mkoani Tanga kwa ziara ya kuzindua mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta amesema hawezi kuvumilia kuona mashamba yakaichwa mapori badala ya kuyaendeleza.

Amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, injinia Robert Gabriel kuwa amefanya vizuri katika suala la ujenzi wa madarasa na ameweza kujenga madarasa mengi kwa kushirikisha wananchi na hivyo kuokoa fedha za Serikali.

“Sina tabia ya kusifia lakini DC wa Korogwe nampongeza na msije mkashangaa mkiona amepanda cheo…ingawa hapa Korogwe mtachukia kwa sababu namuondoa mchapakazi,” amesema Magufuli.

Rais Magufuli alipokewa jana na uongozi wa Mkoa wa Tanga saa 4.37 katika Kijiji cha Makata na baadaye alizungumza na wananchi waliokusanyika katika maeneo ya Kabuku, Michungwani, Hale, Muheza na Mlingano.

Mwananchi

Comments

comments

Exit mobile version