Dar es Salaam. Mshereheshaji maarufu nchini Emmanuel Mathias maarufu Mc Pilipili ameyataja mambo makubwa matatu aliyojifunza baada ya kupata ajali ya gari Septemba 12 mwaka huu katika Kijiji cha Nyasamba mkoani Shinyanga.
Akizungumza na MCL Digital leo, mchekeshaji huyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kuwakwepwa waendesha baiskeli waliokuwa pande mbili tofauti za barabara.
“Nakumbuka mara ya mwisho nilikuwa nachati, ghafla gari ikayumba upande wa kwanza na baadaye ilirudi upande wa pili, ikapinduka ghafla kioo cha mbele kikavunjika mimi nikarushwa kupitia kioo cha mbele nikatolewa mpaka nje, nilifikia kiuno na mashuhuda wanasema waliniona nikidunda dunda sana kutumia mgongo na makalio na pale pale nikaanguka chini na kuzimia,” amesimulia.
Mc Pilipili amesema alizimia kwa siku nne lakini kupitia ajali hiyo amejifunza mambo makubwa matatu ambayo anahisi huenda ni muhimu kwa msanii, mtu maarufu au mwananchi wa kawaida kuyazingatia.
“Wasanii wengi ni vizuri kuwa na miradi mingine ili ukipata ulemavu iweze kukusaidia, mfano ningeangukia mdomo nisingeweza tena kuwa Mc. Ni wakati muafaka kwa wasanii na watu maarufu kuanzisha biashara nyingine ambazo zitazalisha fedha.”
“Nikaona jambo la kuishi bila mke si zuri, siku ambayo nilisema bora ningekuwa nimeoa ni kipindi naumwa mama alinilea kama mtoto, nguo ananivalisha na chakula wananilisha wadogo zangu,” amesema.
Mc Pilipili amesema baada ya kupata ajali alikuwa kimya kwa sababu sehemu ya mwili wake ilikuwa imeathirika ikiwemo kupoteza fahamu, kuumia kwa mguu na mkono wa kushoto na kifua hali iliyomfanya kuahirisha shoo zake zilizokuwa kwenye ratiba.
Amesema katika kuwashukuru Watanzania na watu wa Mwanza waliomsaidia kipindi cha ajali, atafanya shoo itajulikana kwa jina la Stand Up Comedy Tanzania ambapo itafanyika katika mikoa mitatu ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.
“Nina wiki mbili sasa tangu nimeanza kazi za ushereheshaji wa harusi baada ya kukaa kimya kwa sababu ya ajali na hii yote niliamua kutulia ili mwili ukae vizuri hususani katika kazi zetu. Nashukuru Mungu na maombi ya Watanzania kwa sasa nipo fiti na ninakamua kazi zangu kama kawaida,” amesema Mc Pilipili.
By Herieth Makwetta, Mwananchi
Comments
comments