Artists News in Tanzania

Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa Kuwanufaisha Wasanii

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema ipo katika mchakato wa kuanzisha ‘Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa’ ambao utakuwa unawasaidia wasanii kuinua kipato chao.

 Naibu Waziri ,Annastazia Wambura

Hayo yamebainishwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Annastazia Wambura alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Kinondoni, Maulid Said Mtulia wakati alipotaka kujua mipango ya serikali katika kuongeza vifaa, mtaji na usimamizi wa vijana walioamua kujiajiri kupitia sanaa mbalimbali, maonesho ya mitindo na michezo.

“Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iko katika mchakato wa kuanzisha “Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa” ambao una dhima kubwa ya kusaidia kuinua kipato, kuongeza tija na weledi kupitia utaratibu wa upatikanaji fedha utakaowekwa ili kuwawezesha wasanii kuzalisha kazi bora za sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ndani na nje ya nchi”. Alisema Mhe. Wambura

Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo amesema katika kipindi hiki ambacho mfuko huo unaandaliwa, serikali imeshauri halmashauri zote ziweze kuwasaidia vijana wanaojishughulisha na sanaa kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya kupata mitaji kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato kila ya halmashauri kwa kuwa sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wa sasa.

Kwa upande mwingine Spika wa Bunge, Job Ndungai amesema ni bora kuzingatia masuala ya sanaa maana katika mpira wa miguu kumeanza kupotea huku akiwapiga kijembe mashabiki wa timu ya Yanga kuwa walifungwa bao 4 wakaanza kupoteana uwanjani.

“Bora tuzingatie masuala ya sanaa maana huku katika mpira wa miguu watu wamefungwa bao 4 wakaanza kupoteana uwanjani, namuuliza Mhe. Waziri hana majibu” amesema Spika wa Bunge, Job Ndungai

Eatv.tv

Comments

comments

Exit mobile version