Hii ndiyo hali halisi! Ikiwa leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa staa wa filamu Bongo, Steven Charles Kanumba ambapo ametimiza miaka minne kaburini, mambo mbalimbali yametokea tangu alipofariki dunia huku magari na kampuni aliyokuwa akimiliki vikiwa vimepukutika kama majani.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 maeneo ya Vatcan-Sinza jijini Dar nyumbani kwake alikokuwa akiishi ambapo aliyekuwa mpenzi wake kwa siri, staa wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ alishikiliwa na polisi na kusweka katika Gereza la Segerea kwa mwaka mmoja, akidaiwa kuhusika na kifo chake kwani ndiye aliyekuwa naye chumbani usiku huo.
TASNIA YA FILAMU
Tangu Kanumba aondoke, tasnia ya filamu imedorora na wasanii wengi wamekuwa wakikiri kwamba ni kutokana na kifo cha staa huyo kwani ndiye aliyekuwa chachu na changamoto kubwa ambayo ilikuwa ikisababisha wengine kufanya kazi kwa bidii ili wamfikie au pengine wapite kiwango alichoku
wanacho.
TUZO ALIZO-NAZO
Kwa mujibu wa mama Kanumba, Flora Mtegoa hadi sasa marehemu anashikilia tuzo zaidi ya saba alizopewa na wadau wa sanaa hapa nchini kwa kutambua mchango wake tangu alipofariki dunia.
Kutokana na idadi hiyo ya tuzo, hadi sasa hakuna msanii yeyote wa filamu nchini ambaye ameweza kufikia rekodi hiyo.
WASIKIE HAWA
“Kiukweli sanaa ya filamu imepoa sana na imekosa mwelekeo tangu alipofariki Kanumba, unajua alikuwa analeta changamoto ya kila mtu kufikiria atafanyaje ili amfunike Kanumba lakini sasa hivi watu wamebweteka, hakuna anayewaumiza kichwa tena, jambo ambalo limesababisha tasnia ya filamu kupoa na kukosa msisimko kama zamani,” anasema msanii wa filamu, Tiko Hassan.
Naye msanii mkongwe kwenye tasnia ya filamu, Hidaya Njaidi alisema:
“Kanumba alipofariki dunia tasnia ilikufa kabisa, sasa hivi ndiyo inaanza kufufuka kidogo baada ya serikali kuitambua na kuipa sapoti lakini vinginevyo hakuna ambaye ameonekana kuliziba pengo la Kanumba.”
Kanumba na Vincent Kigosi ‘Ray’ walikuwa ni washindani kwa kila kitu, iwe ni magari, blogu na hata katika filamu lakini Kanumba alipofariki dunia, hata Ray mwenyewe alipoa na manjonjo yake hayaonekani kama zamani.
MAGARI NA KAMPUNI
Miaka minne baada ya kifo cha Kanumba, magari yake matatu, Toyota Hiace, Toyota GX 110 na Toyota Lexus ambalo lilifanana na la Ray alilolinunua Sh. milioni 78. Toyota Hiace ambalo lilikuwa ni maalum kwa ajili ya kufanyia kazi za filamu ndani ya kampuni yake ya Kanumba The Great na Toyota Hiace yote hayaonekani. Yanadaiwa kuuzwa na sasa mama Kanumba anatumia usafiri wa daladala.
Isitoshe pia Kanumba alikuwa na ofisi maeneo ya Sinza-Mori, Dar lakini kwa sasa haipo tena na kwa mujibu wa mama yake, vifaa vyote wamehamishia nyumbani kutokana na kushindwa kulipia kodi ya pango.
MAMA KANUMBA ANASEMAJE?
Akizungumza kwa uchungu, mama Kanumba alisema kuwa kuhusu magari, hayapo na anaomba mwanaye aachwe apumzike salama huko alipo kwani anapoulizwa maswali mengi ndipo anazidishiwa uchungu zaidi.
Kuhusu kampuni alisema vifaa vyote vipo nyumbani (Kimara-Temboni) na ikitokea kama kuna kazi ya filamu basi wahusika waliokuwa wanafanya kazi na Kanumba huwa wanakwenda kufanyia hapohapo nyumbani.
VIPI KUHUSU BLOGU YAKE?
Mama huyo alisema kwamba hafahamu chochote kuhusiana na mambo ya mtandao hivyo hajui chochote kuhusu Blogu ya Kanumba the Great.
MDOGO WAKE KANUMBA YUKO WAPI?
Mdogo wa Kanumba anayejulikanakwa jina la Seth Bosco anasema baada ya Kanumba kufariki dunia mama yake ndiye aliyechukua nafasi ya mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mwanaye hivyo hajui chochote kinachoendelea na ikitokea kuna kazi ya filamu huwa anaenda kufanya lakini kwa sasa anajishughulisha na mambo yake binafsi ya sanaa.
Kwa upande wa blogu ya Kanumba www.kanumbathegreat.blogspot.com ambayo picha ya mwisho kuwekwa ilikuwa Aprili 6, 2012 anasema kwamba walishindwa kuiendeleza kutokana na kuwa hawana namba ya siri ‘password’ yake kwani alikuwa nayo mwenyewe Kanumba na hakuna anayeifahamu hadi sasa.
MIRATHI VIPI?
Mama Kanumba anasema suala la mirathi halipo tena na bado yupo anasikilizia kama anavyosikilizia kesi ya Lulu kuanza kutajwa mahakamani ila kama Baba Kanumba, Charles Kanumba ataibuka na kuzungumzia tena mali za mwanaye, ataenda kufungua mirathi.
NINI HATMA YA LULU?
Baada ya kukaa gerezani kwa mwaka mmoja, Lulu aliachiwa huru kwa dhamana baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusikiliza kesi hiyo na kukutwa na kesi ya kuua bila kukusudia, mpaka sasa haijaanza kusikilizwa.
Katika kumbukumbu ya kifo cha Kanumba leo, ibada ya kumuombea itafanyika Kanisa la KKKT, Temboni jijini Dar na baada ya hapo mama yake pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wataelekea Makaburi ya Kinondoni kulifanyia usafi kaburi lake.
Mama Kanumba anasema kwa mwaka huu utaratibu utakuwa ni huo tu lakini kwa mwaka kesho atakapotimiza miaka mitano atamfanyia kitu maalum, hakukiweka wazi.
Chanzo:GPL
Comments
comments