Mike Sangu Afunguka Hatma ya Ndoa Yake na Thea
JINA alilopewa na wazazi wake ni Michael Sangu lakini kwenye sanaa anatambulika kwa jina la Mike. Ni mwigizaji na mwongozaji wa filamu za Kibongo kwa muda mrefu.
Habari kubwa zaidi katika maisha yake kwa sasa ni kuhusu ndoa yake na mwigizaji mwenzake Salome Ndumbangwe Misayo ‘Thea’. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa amekuwa na mgogoro na mkewe huyo, huku wazazi wa pande zote mbili wakihaha kurejesha pendo lao la awali.
Katika kipindi hiki cha giza la hatma ya ndoa yao, hakuna mmoja kati yao aliyepata kuzungumzia hilo mahala popote, hadi juzi Swaggaz lilipokutana uso kwa macho na Mike ambaye alifafanua hilo na mengine kuhusu maisha yake.
NDOA BADO IPO?
“Haipo kaka… tumeachana na uhusiano wetu unaendelea kutokuwa mzuri licha ya wazazi wetu hasa upande wangu kuendelea kufanya juhudi za kutupatanisha.
“Ukweli ni kwamba siwezi kurudiana tena na Thea kwa sababu tatizo tunalijua mimi na siyo wazazi. Naangalia utaratibu wa kutengua ndoa hiyo ili nianze maisha mapya.”
BAJETI YA SIKU IKOJE?
“Kwenye chakula haizidi shilingi 10,000. Asubuhi nakunywa glasi moja ya juisi halisi na vipande viwili vya mkate. Mchana nakula matunda na jioni matunda kidogo, lengo ni kupunguza mwili. Awali nilikuwa nakula kuku mzima lakini sasa nimepunguza, ikitokea siku nakula kuku basi atakuwa nusu.”
KINACHOMKERA ZAIDI
“Nakerwa zaidi na watu waongo na wanafiki. Kwani hawa wanaweza kusababisha watu waliopendana kugombana na kuchukua muda kutambua kwamba jambo lililowagombanisha lilikuwa la uongo ama la.”
WASANII WENGI HUONEKANA MAMBO SAFI, NI KWELI?
“Wengi hupenda kujionesha kwenye jamii kwamba maisha yao ni mazuri kumbe siyo. Wapo wanaokodi magari ya kifahari ya kutembelea na baadhi wanadiriki kukodi nguo za gharama ili waonekane wana pesa lakini nyuma ya pazia ni masikini wa kutupwa.
“Binafsi nachukizwa na hali hiyo kwani si nzuri mtu kama anacho anacho tu na kama hana hata afanyeje hawezi kufanikiwa.”
ANAMILIKI MKOKO?
“Nilikuwa na gari lakini kwa sasa nimeliuza, nikanunua kiwanja, sasa hivi naendelea na ujenzi. Mungu akipenda mpaka mwaka huu ukiisha nitakuwa nimekamilisha nyumba yangu. Nimechoka nyumba za kupanga.
“Safari zangu nyingi natumia daladala na huko nakutana na mashabiki wangu wa filamu. Hata hivyo nina pikipiki lakini huwa siitumii sana.”
ANAPENDA KUFANYA NINI MAISHANI MWAKE?
“Napenda fani hii ya uigizaji lakini zaidi uongozaji. Nafuata nyayo za kaka yangu marehemu George Tyson na sasa kuna kazi naandaa, naamini itakuwa bora kuliko nilizowahi kuzitengeneza.”
Mtanzania