Mimba ya Wema Yayeyuka Ghafla
Mimba ya staa wa filamu Bongo, Wema Sepetu iliyokuwa gumzo kila kona, ni kama puto kwani baada ya kupulizwa, kujaa na kuvuma sana, hatimaye limepasuka na kuacha vilio kwa familia na watu wake wa karibu, Risasi Mchanganyiko linaweza kuripoti.
JIUNGE NA CHANZO
Chanzo chetu makini kilichoomba hifadhi ya jina lake ili kulinda ‘ushosti’ wake na Wema, kimeliambia gazeti hili kuwa mimba ya supastaa huyo, ambayo inadaiwa kutojulikana mhusika halisi, imetoka baada ya kuharibika muda mfupi tangu watoke kujiachia katika viwanja vya maraha jijini Dar.
“Yaani ngoja nikwambie ukweli, ujue juzi hiyo kabla ya mimba kuharibika, tulikuwa naye kwenye sherehe yetu ya Timu Bella ambapo Wema alikuwa safi tu na cha ajabu siku hiyo hata hakunywa pombe kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma.
“Tena tuliambiwa baada ya kupimwa ilionekana mimba yake ni ya watoto mapacha, akawa na furaha sana pamoja na ‘baby’ wake Idris, hivi sasa kila nikifikiria naona ni jinsi gani Wema yupo katika hali mbaya, maana naitazama furaha yake endapo angejifungua salama,” kilisema chanzo hicho.
HOSPITALINI AGA KHAN
Chanzo hicho kiliendelea kudai kuwa hali ya Wema ilibadilika ghafla baada ya kuanza kujisikia vibaya, ambapo tumbo lilianza kuuma na kumpa maumivu makali ambayo yalisababisha damu kuanza kumtoka sehemu za siri, jambo lililowafanya walio karibu naye kumkimbiza katika Hospitali ya Aga Khan, Dar kwa matibabu.
“Alipofika kule ikafahamika kuwa ujauzito wake umeharibika, kilichofanyika ni kumsafisha kama inavyokuwa kwa wajawazito wote wanaoharibikiwa na mimba zao.”
IDRIS, WEMA WAANGUA KILIO
“Sijawahi kuwashuhudia Wema na Idris wakilia kwa uchungu kama ilivyokuwa siku mbili hizi baada mimba hiyo kutoka, ni rahisi kwa watu ambao hawajui hali halisi kuona kama Wema alikuwa akiigiza ila kama ingetokea mtu wa nje angekuwa karibu kama ilivyo kwangu, wasingeweza kumbeza kwa kumwambia hakuwa na mimba.”
MSIKILIZE MADAM MWENYEWE
“Kusema ukweli mimi kwa sasa sijisikii kuongea chochote juu ya hilo maana hata kama nikiongea nini, ukweli utabaki kuwa mchungu kwangu, sipo vizuri hivyo naomba niachwe kidogo, maana hakuna jambo jipya ninaloweza kuliongea hapa likaeleweka zaidi ya kunyamaza,” alisema Wema.
BIBI KIKONGWE ATOBOA SIRI NZITO
Bibi mmoja kikongwe, Atha Magego (70) ambaye alikuwa mkunga enzi zake, alisema kutoka kwa mimba ya Wema kumesababishwa na kelele nyingi na kutotulia kwa mwanamke huyo maarufu.
“Vijana wa siku hizi hawajui miiko, mtu mjamzito hapaswi kuwa mtembezi, hasa mbele ya watu wengi na mbaya zaidi usiku. Dunia ina watu wengi wabaya, wanaweza kufanya lolote hata kama hawafaidiki.
“Kwa mtu maarufu kama Wema, hakupaswa kuwa mtembezi maana kuna macho mengi mabaya, angetulizana nyumbani na ikibidi angekwepa kabisa kuonekana ovyoovyo zaidi ya watu wake wa karibu. Lakini ukiacha hivyo pia, alipaswa kutulia nyumbani ili kuufanya mwili uzoee hali ya ujauzito,” alisema kikongwe huyo.
Chanzo:GPL