Mpasuko,Aslay Kubomoa Team Kiba, Team Diamond Leo?
HITIMISHO la msimu wa Tigo Fiesta unatarajia kuhitimishwa leo kwenye Viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, huku mashabiki mbalimbali wakisubiri kwa hamu kuhudhuria tukio hilo la kihistoria kwenye kiwanda cha burudani Bongo.
Pamoja na kutokuwapo kwa msanii wa kimataifa kama ilivyozoeleka, lakini mashabiki wa burudani wameonekana kuridhishwa na wasanii wa hapa nyumbani ambao soko la ushindani limezidi kujidhihirisha kadiri muda unavyokwenda na kuwafanya wazidi kufanya vizuri.
Licha ya wasanii kama Rostam (Roma na Stamina), Maua sama, Nandy na wengine kufanya vizuri katika msimu huu wa Tigo Fiesta, lakini macho ya mashabiki wengi yanamtazama zaidi kijana mdogo, Aslay ambaye ameonekana kuja kwa kasi zaidi kupitia nyimbo zake, hasa baada ya shoo zake za mikoani kufanya vizuri.
Uwapo wa Aslay katika tamasha la leo, huenda ukawasahaulisha mashabiki wa Ali Kiba na Diamond – uwezo wa nyota hao ambao wote wametoa nyimbo mpya hivi karibuni ambazo zimefanya vizuri na badala yake, wakaelekeza zaidi masikio yao kwa kijana huyo ambaye kwa sasa ni kipenzi cha mashabiki wengi wa muziki hapa nchini.
Ali Kiba kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Seduce Me, huku Diamond akiwa na kibao matata cha Hallelujah, ikiwa ni kolabo na Morgan Haritage, zote zikiwa zimepokewa vizuri na mashabiki.
Akitamba na nyimbo zake mpya za Pusha, Natamba, Mario, Danga, Rudi, Kidawa na nyinginezo, Aslay anatajwa kuwa msanii aliyeongoza kwa kupewa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wakati wote wa tamasha la Tigo Fiesta ambapo mashabiki walikuwa wakiimba naye na kucheza nyimbo zake kwa hisia kali.
Kukosekana kwa Diamond katika tamasha la leo, huku Ali Kiba akiwapo, kunaweza kufungua mlango kwa Aslay kupata sapoti zaidi kwani hakutakuwapo ushabiki wa Team Kiba na Team Diamond kama ilivyojitokeza katika matamasha yaliyopita.
Akizungumzia tamasha hilo lenye kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema:
“Kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2017 kitawahusisha wasanii wa Kitanzania pekee. Tigo imejikita kuleta mageuzi makubwa kwa kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa na ajira kwa vijana nchini. Tumewakutanisha wasanii wetu maarufu na mashabiki wao katika mikoa yote 16 tuliyotembelea na kuwajengea uwezo wa kutumbuiza laivu mbele ya halaiki kubwa ya watu.”
Alisema wameamua kutumia wasanii wa ndani kwani wameona wana uwezo wa kukata kiu ya muziki ya Watanzania bila hata kuwa na msanii kutoka nje ya nchi.
SEBASTIAN MAGANGA ATIA NENO
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandilizi ya Tigo Fiesta 2017, Sebastian Maganga, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi Leaders Club akiwaahidi kupata burudani ya hali ya juu, huku pia akiwahakikishia ulinzi wa kutosha, hasa wakati wa kutoka.
“Tamasha la Tigo Fiesta litaanza mapema tu, milango itafunguliwa saa sita mchana na kutakuwa na matukio mbalimbali yanayolingana na muda huo na itakapofika saa moja jioni, moto utawashwa rasmi kwa wasanii kuanza kulishambulia jukwaa kama nyuki hadi saa saba usiku,” alisema Maganga.
LISTI HII HAPA
Maganga aliwataja wasanii watakaotoa burudani leo katika tamasha hilo kuwa ni Ali Kiba, Aslay, Ben Pol, Barnaba, Chege, Darassa, Dogo Janja, Jux, Fid Q, Rostam (Roma na Stamina), Rich Mavoko na Nandy.
Wengine ni Mr Blue, Vanessa Mdee, Maua Sama, Zaiid, Lulu Diva, Mimi Mars, Rosa Ree, Chid Beez, Nyandu Tozi, Nedy Music, Ommy Dimpoz, Bright, Weusi (Joh Makini, G Nako na Nikki wa Pili) na wengineo.
Alisema kuwa tamasha hilo kwa mwaka huu limezunguka katika miji ya Arusha, Kahama (Shinyanga), Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea (Ruvuma), Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi (Kilimanjaro) na Mtwara.
WASANII WALA KIAPO
Ben Pol, mmoja wa wasanii watakaopanda jukwaani leo Leaders Club akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema wamejipanga vilivyo kufanya mambo makubwa, kila mmoja wao akiwa amepanga kufanya surprise ya aina yake itakayokamilisha msimu wa Fiesta mwaka huu kwa aina yake.
Naye Vanessa Mdee, alisema: “Wakazi wa Dar es Salaam watarajie shoo kabambe zaidi ya ilivyokuwa mikoani, kwa upande wetu wasanii tumejipanga kufanya shoo kali, hatutawaangusha hata kidogo.”
Kwa upande wake Aslay, dogo anayetazamiwa kufanya maajabu leo, amesema: “Jumamosi (leo) pale Leaders Club, Dar es Salaam ndiyo kilele cha Tigo Fiesta, nimejipanga kufanya mambo makubwa hivyo wapenzi wa muziki na burudani wajitokeze kwa wingi wafaidi burudani ya nguvu.”
Mtanzania