MASHABIKI wa muziki wa kizazi kipya nchini wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya ukimya wa Tip Top Connection na kuamini limekufa baada ya bosi wao, Babu Tale kukimbilia WCB kupiga hela.
Rais wa Manzese, Madee amemkingia kifua bosi wake huyo na kufunguka kuhusu kundi hilo lililowaibua nyota mbalimbali wanaotamba nchini kwa sasa.
Madee anasema watu wajue kabisa kuwa, Tip Top haijafa na Babu Tale anaendelea kuwa bosi wao kama kawaida licha ya kuonekana yupo bize na mambo ya Diamond Platinumz.
“Muziki wa makundi haulipi, ndio maana hata kwa sasa wengi wanaona kama Tip Top limekufa au limesaliwa na wachache, ila ukweli kundi lipo na linaendelea kama kawaida ila lipo kimya kwa kuwa kila mtu anafanya kazi kivyake,” anasema.
Anasema kundi lina wasanii watatu Madee, Dogo Janja na Tundaman na bosi ni Babu Tale, baada ya wasanii wengine kuondoka kusaka maisha kwingine.
BIFU KIZAMANI
Madee aliwahi kuingia kwenye mzozo wa maneno baada ya kutoa ngoma yake ya Hiphop Hailipi na kisha kudaiwa amewahi kukwaruzana na Nay wa Mitego kisa ikiwa kugombea Urais wa Manzese.
Hata hivyo, mkali huyo wa ‘Pombe Yangu’ anasema bifu ni mambo ya kizamani na kwamba hajawahi kuwa na bifu na wenzake, ila walitofautiana kauli tu katika masuala mazima ya kupeleka muziki wa Tanzania mbele.
“Sijawahi kuwa na bifu na Nay wa Mitego, tulitofautiana kauli tu, haitatokea niwe na bifu na msanii yeyote sio wa Mitego ambaye kwangu ni mdogo kwani amenikuta kitambo naimba,” anasema.
Akizungumzia muziki wa Nay, Madee alidai ni mzuri kwa vile anafanya tofauti na wengine na anasema kile anachokiamini ni sahihi.
KIKATUNI CHA WOLPER
Katika kazi yake ya Sikila kuna kikatuni kilichoibua maneno baina yake na Jackline Wolper, Madee anafafanua.
“Nimesikia tetesi hizo kuwa Wolper anadai anahusika katika ile video, lakini ukweli ni kuwa ile katuni sio yeye, kwanza yeye sio katuni, ule ni mfanano wa dada mmoja ambaye yupo Nigeria,” anasema na kuongeza;
“Nilipanga tangu muda sana kwa staili hiyo miaka kama mitano iliyopita, lakini kwa kipindi nawaza nifanye kitu kama hiki teknolojia, gharama pia ilikuwa ni tatizo.”
“Mwaka huu nilivyoona kuna mtu amechora katuni nzuri Instagram nilimfuata Direct Message (Dm), kisha nikamwomba namba, halafu nikamtag Babu Tale alipoona aliniuliza, nikamwambia hiki kitu ninacho muda mrefu ndio akaniambia tufanye kwa wimbo gani, nikamwambai huu niliofanya na Tekno.”
Madee anasema kitu kingine ambacho kilimfaya afanye kitu tofauti ni baada ya kuona karibu wasanii wote nchini wakifanya kitu kile kile, magari mazuri, boti za baharini, nyumba nzuri yeye aliamua kuja kivingine kabisa.
MAPOKEO KWA WADAU
Madee anafunguka kuwa mashabiki wake wamekuwa na mapokezi ya tofauti na nyimbo zake zote, huku akisema kuwa wimbo huo umepokelewa tofauti kabisa huku watu wakimshangaa kwa kile ambacho amekifanya.
“Huwezi kumzuia mwanadamu asiongee, ilikuwa ni lazima watu waongee na mimi nilitaraji kwa sababu ni kitu kigeni, lakini mbona hiki kitu Ulaya kilifanywa zamani na 2Pac na Kanye West kwenye nyimbo zao kubwa na bado nyimbo zao zilitamba,” anasema.
USHAURI WAKE
Madee amewageukia wakongwe wenzake na kuwapa ushauri huu;
“Wakubali mabadiliko, ukiwa kila siku unafanya kitu kile kile watu walichokizoea kukuona inafanya wakukinai, hivyo wenzangu wabadilike ili kwenda na kasi ya ushindani iliyopo kwa sasa,” anasema.
“Hata kama unakuwa una rap basi unaangalia na kuweka vikolombwezo ambavyo vitakufanya uwe wa kitofauti, hata sasa hivi tunaona kabisa hao walioanzisha muziki huu, wao wenyewe wameogezea ladha,” anasema.
NGOMA KALI
“Katika kazi zangu nilizowahi kufanya ‘Kazi Yake Mola’ ndio ngoma nisiyoweza kuisahu. Niliifanya kwa ubora sana na hata leo nikiusikiliza hakika huwa nahisi kama sio mimi vile na bado unaendelea kutumika sehemu yoyote,” anasema.
“Zamani kupata nafasi ya kurekodi, ilikuwa kazi, ndio maana ukipata nafasi ya kurekodi ilikuwa lazima uitumie kwa nguvu na maprodyuza pia walikuwa wawili tu ambao walikuwa wanafanya kazi nzuri hivyo ili upate nafasi ya kufanya nao kazi ilibidi ujitutumue.”
TUKIO BAYA
“Sitosahau nilipotoa wimbo wa Hiphop Haiuzi, nikapata shoo Morogogo nilifanyiwa fujo kubwa sana, watu walitupa machupa wengine wakawa wanarusha vitu stejini lakini nashukuru sikuumia na hakuna mtu aliyezurika ila pia sitosahau siku niliyotoa wimbo wa Nani kamwaga pombe, kwa jinsi ilivyopokelewa na watu ilikua ni hatari sana, ila mimi wakati nafanya niliona kazi ya kawaida, kiukweli siwezi kusahau,” anasema.
UHUSIANO
Madee anakiri wazi kuwa kwenye uhusiano, lakini hayupo tayari kumtaja kwa vile hata huyo mpenzi wake, hataki kutajwa ila wakati ukifikia watu watamjua.
“Bado hataki hata yeye kufahamika na watu ila wakati ukiwadia watu watamfahamu shemela yao na ikiwezekana watu wanaweza kushuhudia ndoa pia sio muda sana,” alisema.
Madee amemfagilia Rayvan akidai sio wa mchezo mchezo;
“Rayvany sio msanii bali ni mwanamuziki, yule anaweza kupiga gitaa, kuimba kwaya, kupiga ngoma na mambo mengine yote ambayo mwanamuziki anatakiwa awe nayo, hivyo niliona yeye aende tu Wasafi na tangu ameenda amesogea na kila mmoja anaona kitu ambacho anakifanya,” anasema.
MAFANIKIO YAKE
“Kwa mafanikio ya kujivuni ni kuongeza marafiki, pia kumsomesha mtoto wangu shule nzuri, nalipa ada kwa mwaka Sh6 milioni, kwa nini nisijivunie muziki?
“Siwezi kutaja mafanikio ya magari kwa vile ni vitu vya kupita, lakini ni muziki ulionifanya leo nitembelee gari, lakini huwa sikai na gari muda mrefu kila mara nauza na kununua jingine.”
Mwanaspoti
Comments
comments