Msondo Yamdai Mamilioni Diamond
WIMBO wa Zilipendwa ulioimbwa na waimbaji wa WCB na kujipatia umaarufu mkubwa, umeiponza lebo hiyo baada ya bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma kudai fidia Sh300 milioni.
Msondo inalalamikia kitendo cha WCB kutumia sehemu ya kazi yao katika wimbo huo uliimbwa na wasanii Harmonize, Diamond, Maromboso, Rich Mavoko, Lavalava, Queen Darleen na Rayvanny kinyemela bila idhini yao.
Kupitia kampuni ya Uwakili ya Maxim Advocates, Msondo inailalamikia WCB kutumia sehemu ya wimbo wao wa Ajali katika singo yao ya Zilipendwa bila kupata idhini yao ambayo ni kinyume na sheria ya hakimiliki.
Kwa mujibu ya notisi waliyoiandikia WCB ya Novemba 7 na iliyosainiwa na mmoja wa Mkurugenzi wa Maxim, Mwesigwa Muhingo, wimbo wa Zilipendwa umejipatia umaarufu mkubwa na kuinufaisha lebo hiyo kifedha bila Msondo kuambulia chochote kwa kutumiwa kwa mirindimo ya saxafone iliyotumika katika wimbo wa Ajali.
Kama WCB itashindwa kutekeleza agizo hilo, kampuni hiyo kwa niaba ya Msondo itachukua hatua zaidi ili kuhakikisha wanapata haki yao kwa lengo la kufanya wasanii kuheshimu kazi za wenzao na sheria ya hakimiliki.
Wakati hilo linaibuka kwa sasa tayari mmoja wa mameneja wa Diamond, Babu Tale ambaye pia ni bosi wa Tip Top Connections mali zake zipo mbioni kupigwa mnada kutokana na kosa la hakimiliki za kazi za Sheikh Hashim Mbonde.
Kadhalika kampuni ya mtandao wa simu za mkononi, Tigo ikihukumiwa kuwalipa Sh2 bilioni wasanii AY na MwanaFA kwa kutumia kazi zao bila ridhaa yao.
Mwanaspoti