Bwana Edwin Bruno, mjasiriamali wa Kitanzania, mshindi wa tuzo ya kijana mwenye mafanikio 2015, mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya Smart Codes (www.smartcodes.co.tz) ametajwa katika jarida la Forbes Africa. Kila mwaka, jarida hilo hutoa orodha ya vijana 30 wenye umri chini ya miaka 30 ambao wana nafasi ya kuwa mabilionea wa baadaye.
Majina hayo yalikusanywa na kuandaliwa na mhariri wa Forbes Afrika, Ancillar Mangena ambaye naye ana chini ya miaka 30. Katika ujumbe wake, anaandika “Orodha inawakilisha vijana ambao tunaamini wana uwezo wa siku moja kuwa kwenye ukurasa wa mbele wa jarida la FORBES AFRICA, ikimaanisha watakuwa na thamani halisi ya si chini ya dola za kimarekani milioni 200, wameajiri maelfu ya watu na kusaidia kukua bara la Afrika.”
Katika mazungumzo mafupi na Edwin Bruno, anasema “Nimepewa heshima kubwa kuwa kwenye orodha hiyo, hata hivyo hii inatokana na juhudi za timu nzima pale Smart Codes. Ni wao ndio wanaofanya kazi kubwa, ambayo inaonekana ndani nan je ya nchi”
Kuhusu mafanikio yake mengine, Bruno anasema “ Ni kweli, mwaka jana programu yetu ya m-paper, ambayo inakupa nafasi ya kusoma magazeti ya Tanzania…sio vichwa vya habari, ila gazeti lote kutokea ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho kwenye simu yako au kompyuta ilishinda tuzo ya Best Educatinal Innovation Africa, au kwa Kiswahili tuzo ya uvumbuzi bora wa kielimu barani Afrika.”
Bwana Bruno alimalizia kwa kuonesha furaha yake na kuwasihi vijana wengine kufanya kazi kwa kujituma ili waweze kufikia malengo yao au kama yale aliesema mhariri wa Forbes Africa Ancillar, kusaidia kukua kwa bara la Afrika kiuchumi.
Comments
comments