Mwanafunzi Ajirusha Ghorofani
Mtoto anayedhaniwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya DYCCC iliyopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam amejirusha kutoka ghorofa ya nne mpaka chini huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijafahamika haraka.
Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Temeke, Andrew Satta amekiri kutokea kwa tukio hilo ingawa taarifa hizo zipo kwenye mitandao na hazijafikishwa kituoni hapo, lakini tayari wameanza kufuatilia ili kubaini nini chanzo cha cha tukio hilo.
“Ni kweli tumeona hilo tukio hata sisi kwenye mitandao ya kijamii lakini bado hatujapata taarifa za awali na tukio bado halijaripotiwa polisi. Sisi tumechukua hatua za kuanza kufuatilia na tukishafahamu tutaweka wazi” alisema Kamanda Satta.
MUENDELEZO
Meneja wa shule ya DYCCC (jina halijafahamika) amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukanusha kwamba mtoto huyo siyo mwanafunzi wa shule hiyo na kwamba alikwenda kusherehekea sikukuu ya Idd kwani ni utaratibu wa wa shule hiyo kuombwa uwanja kwa ajili ya sherehe kila mwaka.
“Nipo nje ya Dar es salaam, lakini anayeonekana kwenye hizo video si mwanafunzi wa shuleni kwetu. Ni mtoto ambaye ametoka Morogoro na kuja Dar es salaam kwa ndugu zake. Alipofika alijumuika na wenzake kusherehekea sikukuu. Sasa kwa tukio hili waandaji watakuwa na majibu mazuri kuliko sisi, kwa sababu wao huwa wanatuomba uwanja na sisi tunawapatia. Lakini mtoto aliokolewa yupo salama na wazazi wake” alisema Meneja wa shule ya DYCCC.
Hata hivyo jina na umri wa mtoto huyo bado havijafahamika.