Mwarobaini wa Wasanii Feki Waja
KATIKA kile kinachoelezwa ni kuhakikisha heshima ya wasanii wa filamu inarejea nchini, Chama cha Wasanii wa Filamu Tanzania, kimelazimika kutunga sheria ya kuwataka wasanii, maprodyuza na wapiga picha wote kujisajili kwenye chama hicho na mtu hatoruhusiwa kufanya kazi bila kujisajili.
Akizungumza jana na MTANZANIA, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Maprodyuza Tanzania, William Mtitu, alisema kuwa kuanzia sasa ni kosa la jina filamu yoyote kuingizwa sokoni iliyochezwa na wasanii wasiojisajili na itaondolewa bila wahusika kufidiwa gharama waliyopoteza wakati wa kuiandaa.
“Kuna watu wengi wenye tabia mbaya wamejiingiza kwenye sanaa kama kivuli cha kufanyia maovu yao hali inayopelekea tasnia hii ionekane ni ya wahuni, hivyo kila msanii anatakiwa kusajiliwa na akifanya mambo kinyume na maadili anafungiwa kufanya kazi ndani na nje ya nchi lengo ni kurejesha heshima ya sanaa hiyo,” alisema Mtitu.
Mtitu ambaye pia ni msanii wa filamu, aliwataka wasanii wote kujisajili katika chama hicho ambacho ndicho chenye jukumu la kusimamia mienendo yote ya wasanii wa Tanzania.
Mtanzania