Artists News in Tanzania

Mwasiti: Nimepania Kuwafunda Mabinti

UNAPOWATAJA wasanii wa kike waliowahi kupata majina makubwa katika muziki wa Bongo Fleva, huwezi kukosa jina la Mwasiti Almasi. Mpaka sasa Mwasiti bado anatesa kwenye muziki huo.

Mwasiti amewahi kutamba na wimbo wa ‘Nalivua Pendo’ ambao mwaka 2009 ulipata tuzo ya Wimbo Bora wa Zuku Rumba katika Tuzo za Kili.

Swaggaz imepata wasaa wa kupiga stori na msanii huyu ambaye kwa sasa ngoma yake ya Unaniangalia inasumbua kitaani.

Tuwe pamoja…

SWAGGAZ: Umefikisha miaka 10 kwenye game sasa, ipi siri ya kudumu kwenye gemu kwa muda mrefu wakati wasanii wengi wa kike huishia njiani?

MWASITI: Ni kweli nimefanya muziki kwa muda mrefu sana, ni miaka kumi sasa. Sababu ni nyingi lakini kubwa ni kuheshimu muziki kama kazi.  Sichukulii kama sehemu ya kupoteza muda, nafanya kama sehemu ya  maisha yangu.

SWAGGAZ: Vigingi gani umepishana navyo kwenye tasnia ya muziki mpaka kumtengeneza Mwasiti anayejulikana kimataifa?

MWASITI: Tangu nianze muziki mpaka sasa yapo mambo mengi ambayo kama mwanamuziki, mfanyabiashara na mwanamke yalikuwa changamoto kwangu; dharau kwa baadhi ya watu na uoga. Nilikuwa muoga wa kuthubutu kwakweli.

SWAGGAZ: Unazungumziaje hali iliyopo sasa ya wasanii ambao walikuja nyuma yenu kuonekana kulishika zaidi gemu?

MWASITI: Kizazi changu mimi sikuwa na akina dada Jide, hivyo kizazi cha akina Vannesa Mdee hakiwezi kufanana na cha kwetu. Lazima kuwepo na utofauti, lakini pia hawa wa sasa wamekuja kupata muda mzuri zaidi tofauti na muziki wa miaka ya nyuma.

SWAGGAZ: Wimbo upi ulisskupatia mafanikio makubwa zaidi?

MWASITI: Nalivua Pendo ni wimbo ambao ulinipa mafanikio na siwezi nikausahau, ulibadilisha karibu asilimia 100 ya maisha yangu hasa kutokana na kunipa tuzo.

SWAGGAZ: Umeifanyia nini jamii kupitia kipaji chako?

MWASITI: Huwa nafanya vitu vingi kama kurudisha kwa jamii na si lazima ninunue vitu… nimekuwa Balozi kwa mambo mengi sana hasa elimu ambapo nimekuwa nikipata nafasi ya kukaa na watu kubadilishana mawazo na kutengeneza picha mpya ya maisha ya baadaye.

Kwa sasa mimi ni Balozi wa Hassan Maajar Trust inayoshughulika na elimu na madawati nchini ambapo kupitia project hiyo nimefanya kazi na Haki Elimu na NSSF na nimeweza kuwafikia vijana wengi nchini.

Ili kudhibitisha kwamba napenda kujitolea kwa jamii katika siku za hivi karibuni natarajia kufungua NGO’s ya mambo ya elimu na ninaamini nitaifikia namba kubwa ya vijana wa Tanzania.

SWAGGAZ: Ipo mifano mingi ya watu kufungua NGO’s halafu zinakuwa za upigaji. Kwako itakuwaje?

MWASITI: Lengo langu ni kuwatoa vijana sehemu moja na kuwapeleka  nyingine kupitia elimu itakayokuwa naitoa maana wapo watu wanatamani kufika mahali nilipo lakini hawajui namna ya kufika… hii haitakuwa mara yangu ya kwanza kwa sababu nimefanya kazi na Sister Tanzania na nimepata uzoefu wa kutosha.

Mfano kuna mambo ambayo kama msanii nikimwambia mtoto inakuwa rahisi kutekeleza kuliko akiambiwa na wazazi wake.

SWAGGAZ: NGO’s hiyo itadili na watu gani hasa?

MWASITI: Nitadili na wanawake wenzangu, kwasababu kwao inakuwa rahisi zaidi kutoa elimu. Ningependa iwe kwa wanaume pia lakini kama unavyojua tena, yapo mambo ambayo mimi kama mwanamke ni vigumu kumwambia mwanaume.

SWAGGAZ: Mwanzo ulizungumzia kuhusu Sisters Tanzania. Je, hiyo inajishughulisha na kitu gani?

MWASITI: Sisters Tanzania nia yake kubwa ni kuwatengenezea mabinti kujitambua na kujiamini, pia sisi kama dada zao tunakuwa tunawaambia mambo ambayo kwa namna moja au nyingine tuliyapitia tusingependa wao wayapitie.

Labda katika umri wetu hatukupata nafasi ya kuambiwa hivyo vitu lakini sisi tumeviona na vinaweza kuwa na madhara kwanini tusikae nao kuwaambia bila gharama yoyote? Tuna daktari anawapima magonjwa yote, pia mwanasaikolojia anayewapa ushauri. Kwakweli nimedhamiria kutoa elimu hii bure kwa wadogo zetu. Ndiyo lengo langu kuu.

Mtanzania

Comments

comments

Exit mobile version