Ni jambo la kawaida kwa wasanii wa kike hapa kujipamba wakati wa kutengeneza video zao kwa mapambo ya kila aina ikiwamo vipodozi.
Hali hiyo inafanya wengine hata kusahaulika sura zao halisi, hasa pale wanapozidisha mapambo hiyo ikiwemo kubadili nywele zao kwa kuvaa za bandia.
Lakini kwa Nandy ambaye jina lake halisi Faustina Charles naona hali hiyo kaibadili katika video ya wimbo wake wa Kivuruge unaotesa kwa sasa.
Mbali na Kivuruge pia katika video ya wimbo wa Subalkheri, alioshirikishwa na Dogo Aslay nao ameonekana kuendelea na mwendo huo huo ambao hadi kufika mwanzoni mwa wiki hii ulikuwa na jumla ya watazamaji zaidi ya milioni.
Msanii huyo anayejiita African Princess, ukiangalia nyimbo hizo mbili zinaakisi jina lake kutokana na namna alivyojiweka Kiafrika zaidi.
Nandy aliyeanza kutambulika na kibao cha Nagusagusa, baadaye One Day, Wasikudanganye, kote humu hajaweza kutendea haki uhalisia wa maisha ya mwanamke wa kiafrika kama ilivyo kwa nyimbo hizo mbili.
Wimbo wake wa Kivuruge ulioonesha maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika na wa Kibongo kwa ujumla kuanzia nyumba anayoishi na mavazi yake.
Kwa wale wanaoishi Uswahilini, vazi la dera ndio mparo mkubwa sio kwa kushindia nyumbani tu, bali hata kutokea kitu ambacho Nandy kakionesha katika video hiyo.
Pia magauni ya mpira maarufu ‘Dar Combined’ yaani ukikatiza kona ya nyumba yako unaweza kuwakuta watu wengine sita wamevaa kama wewe na ukajiona ndio unakwenda na wakati.
Kingine kilichonesha Uafrika Princess ni Nandy kutopaka vipodozi vya aina yoyote katika video hiyo, kwani tumezoea kumuona akiwa na kucha ndefu za kubandika zikiwa zimekolezwa na rangi juu yake lakini kwa kivuruge hakuna hiki kitu.
Pia, suala la mwanamke kuchota maji kazi ambazo mwanamke wa Kiafrika ndizo hasa huzifanya achilia mbali wale waliovutiwa mabomba nyumbani kwao.
Jingine ni ile ya kubeba mfuko maarufu kwa jina la ‘Shangazi Kaja’ pale alipochosha na vituko vya mme wake vya kuwa na vimada. Mifuko hiyo ndio wengi huko Uswahilini wanaotumia kama mabegi yao ya kuhifadhia nguo.
Pia nyumba anayoishi Nandy, ndio familia nyingi za kibongo zenye maisha ya kawaida zinaishi, nyumba ambazo hata gari la wagonjwa au gari la zimamoto kupita ni kazi.
Ndani ya nyumba hiyo ya Nandy na mumewe kwenye korido kunaonekana kuwa na ndoo kibao za kuhifadhia maji, kwa wale waliopanga Uswahilini wanaelewa hii mambo, sasa ole wako ufumwe unachota maji ya mwenzako.
Mtaa ambao Nandy anaonekana kuishi, watu wapo busy na biashara zao za kuuza vitafunwa mbalimbali, mambo ambayo ni adimu kuyaona Uzunguni.
Tukija kwenye wimbo wa Subalkheri, Nandy kaendelea na utaratibu huo, amevaa nguo ambazo msichana wa Kitanzania anakuwa katika maisha ya kawaida hasa vijijini.
Katika video hiyo Nandy anaoneka akiwa amesuka mabutu yake mawili, hajapaka vipodozi usoni na hata maeneo ambayo yupo na mpenzi wake ni ya asili ambayo yanapatikana nchini kwetu hususani maeneo ya Pwani.
Kuna mahali anaonekana akiwa anagema nazi, zao linalopatikana maeneo ya Pwani, pia nyumba waliopo ya udongo inaakisi maisha ya Mwafrika na kuna wakati wanaonekana wakishiriki katika ngoma zinazochezwa huko Uswahilini kwetu na sio kwenye klabu kama ambavyo wanafanya wanamuziki wengine kwenye video zao.
Nandy afunguka ilivyokuwa ngumu kukubali
Akizungumza na mwananchi kuhusu hilo, Nandy anakiri kwamba awali ilikuwa ngumu kukubali kupigwa picha akiwa katika hali ile na kuongeza kwamba anashukuru wimbo huo umeweza kufanya vizuri kwani mpaka sasa umepata watazamaji zaidi ya milioni 1.9 kwenye mtandao wa Youtube.
Anasema ugumu zaidi ulikuja ukizingatia kwamba katika video zake nyingine amejipamba, lakini anashukuru kupitia kivuruge watu wameweza kumjua Nandy halisi ndio nani.
Kuhusu gharama anasema ilikuwa ni rahisi ukilinganisha na video alizozifanya huko nyuma kwani haifiki hata milioni mbili, kwa kati nyingine hadi tano zinafika.
Kwa upande wa mazingira aliyochukulia picha ambayo ni maeneo ya Mwananyamala, anasema anashukuru wananchi walimuheshimu na kuendelea na shughuli zao hali iliyoongeza uhalisia zaidi.
Comments
comments