Artists News in Tanzania

Natasha alivyojigeuza kioo cha Monalisa

Hivi sasa wanawake wengi wamekuwa wakiogopa kuwaruhusu watoto wao hususani wa kike kuingia katika sanaa kutokana na namna wanavyobadilika kitabia wanapokuwa ndani ya ya tasnia hiyo.

Pamoja na uoga huo, kwa Suzan Lewis maarufu kwa jina la Natasha, hakuhofia hilo na kumruhusu mwanae Yvonne Cherry ‘Monalisa’ kuingia ndani ya fani hiyo iliyojaa mitihani kibao kwa watoto wa kike.

Anasema cha kwanza kabisa maji hufuata mkondo, ambapo yeye kama mama amejitahidi kuishi katika maisha ya heshima na hivyo hata Monalisa anapotaka kufanya jambo baya anajiuliza mbona mama hajafanya hivyo.

Jingine lililomsaidia kumfanya Monalisa awe na heshima hadi hii leo ukilinganisha na baadhi ya wasanii ni namna alivyokuwa akifuatilia nyendo zake kwa kila alichokifanya.

Anakiri kuwa wazazi wamekuwa wakiogopa kuwakaripia watoto wao hasa wanapoanza kuwa na majina kwenye sanaa jambo ambalo sio sahihi.

“Unavyomuona Monalisa hadi leo akifanya kitu ambacho mimi sipendezwi nacho namkanya kwa kuwa naamini mtoto kwa mama hakui, na yeye kuwa staa hakunizuii mimi kama mzazi kutekeleza jukumu langu kwake kwa kuwa anapoharibikiwa katika jamii wa kwanza kunyooshewa kidole ni mama,” anasema.

Anabainisha kwamba mahali ambapo wazazi wengi wanakosea kuwaweka katika reli watoto wao ni kwenye umri wa kukua ambapo hapo wengi hupenda kuiga mambo ikiwemo kwa kuyaona kwa watu wengine au makundi anayoongozana nayo.

Akitolea mfano anasema Monalisa ilifika wakati anataka kuvaa kama Wazungu yaani kaptura fupi, sketi, lakini hakusita kumkanya na kumwambia hayo sio mavazi ya heshima na alimsikiliza na kurudi kuzivua jambo ambalo wazazi wengi wanaogopa kulifanya kwa kuogopa kumuudhi mtoto.

Nini kinachowashinda kina mama kwenye malezi?

Natasha anasema moja ya tatizo la kina mama kushindwa malezi ya watoto wao kwa sasa ni mfumo wa maisha, ambapo wazazi wamekuwa busy kutafuta maisha ili mtoto aweze kusoma shule nzuri, kula vizuri na kuvaa vizuri. w“Hivyo mara nyingi unakuta watoto wanashinda nyumbani na wasichana wa kazi, ukirudi huko ilimradi umemkuta kala, kashiba na kalala unaona sawa kumbe kuna vitu unaviacha katika kutekeleza wajibu wako kama mzazi.

“Jambo linalopaswa kufanya katika hili ni kuhakikisha tunatenga muda wetu wa kuzungumza na watoto na wa kutafuta maisha, kwa kuwa jambo la kutafuta fedha halina mwisho na ukijikita zaidi huko unaweza kumkuta mtoto wako keshaharibika na kumrudisha katika mstari ikawa kazi,” anasema mama huyo.

Kuhusu wanawake ambao wanawategemea watoto wao kimaisha kutokana na sanaa na kisha kuogopa kuwakemea kisa tu wanaweza wakakosa kuhudumiwa;

Natasha anasema jambo hilo halina mashiko kwani mtoto huyo pia anapaswa kujua mama yake alicha vitu vyote akamlea yeye, hivyo kupata isiwe sababu akikanywa jambo baya na mazazi ndio azire.

Wakati kwa wakina mama nao wasiogope kutekeleza wajibu wao vyovyote itakavyokuwa kwani wao wamewatangulia hivyo wanajua mengi na wanapomuonya mtoto sio kwamba hawampendi bali ni kumuelekeza katika njia iliyo njema hata kesho aweze kuheshimika mbele ya jamii.

Ilikuaje akamkubalia Monalisa kuigiza?

Natasha anasema anakumbuka Monalisa alikuwa kila siku akimwambia anapenda kuigiza, lakini hakumuamini kama anaweza.

Hata hivyo, anabainisha siku moja wakiwa kanisani, alimshuhudia akiwa anacheza igizo na wenzake na yeye kuonekana kufanya vizuri kuliko watoto wote.

Katika igizo hilo wengi walishangazwa na namna ambavyo aliweza kushika mistari yote aliyoandikiwa na kuiigiza barabara kama ilivyotakiwa na kuanzia hapo akagundua kuwa mwanae kweli ana kipaji na kuanza kumruhusu kwenda kufanya naye mazoezi kwenye kikundi cha Nyota Assemble alichokuwa anaigiza.

Katika kikundi hicho kulikuwepo na wasanii kibao, kwani mbali na Natasha na Monalisa alikuwemo Jacob Steven’JB’, Single Mtambalike”Rich’, Bishanga, Aisha, Waridi na wengineo ambao waliweza kutingisha na maigizo yao yaliyokuwa yakirushwa katika kituo cha televisheni cha ITV.

Katika waigizaji watano waliofanya vizuri Monalisa alikuwa mmoja wapo na ndio wasanii wa mwanzo walianzisha soko la filamu kwa kushiriki kucheza filamu ya Girlfriend iliyoongozwa na aliyekuwa mume wake marehemu George Tyson.

Comments

comments

Exit mobile version