UKISIKIA staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki (Nay wa Mitego) amechia ngoma mpya ni lazima utaitafuta ili usikie kilichoibwa na rapa huyo hata kama huna mapenzi na muziki. Bosi huyo wa lebo ya Free Nation ametengeneza mazingira ya kusikilizwa na mashabiki wake tofauti na wasanii wote.
Mapema wiki hii rapa huyo anayetamba na ngoma yake mpya inayoitwa, Makuzi alitia timu mjengoni (Sinza Kijiweni, Dar es salaam) ambapo alijibu maswali kadha wa kadha yanayohusu muziki na maisha yake kama alivyoulizwa na ripota wa Swaggaz, mastori yalikuwa hivi….
VIDEO VIXENS WENYE MAUMBO….
Katika video za Nay wa Mitego, amekuwa akiwatumia warembo wenye maumbo makubwa ya kibantu. Hiyo imeonekana katika nyimbo kama Shika Adabu Yako, Akadumba, Acheze na hivi sasa Makuzi, rapa huyo ametoboa siri ya kuwatumia ‘mavideo vixen’ wenye maumbo tata.
“Unajua ukimuweka msichana mwenye umbo la kuvutia katika video watu wanapenda, fuatilia video zote zilizofanya vizuri duniani utagundua ndani yake kuna wasichana, hiyo ndiyo sababu inayofanya na mimi niwatumie kwenye video zangu,” anasema Nay wa Mitego.
YOUNG KILLER, GIGY MONEY
Juni 21 mwaka huu Nay wa Mitego aliachia wimbo unaoitwa Moto ambao ndani yake alimzungumzia rapa, Young Killer ambapo alidai amefulia na safari ya kurudi kwao Mwanza inanukia. Killer alimjibu lakini Nay wa Mitego hakujibu tena.
Hali kadharika mwezi Februari mwaka jana, Gigy Money alilalamika kutolipwa fedha yake baada ya kushiriki kwenye video ya Shika Adabu Yako, hapa Nay wa Mitego anafunguka ukweli ulivyokuwa.
“Unajua ukiwa baba huwezi kubishana na mtoto wako, wote mtaonekana hamna akili kwa hiyo ilinibidi nikae kimya ndiyo maana sikumjibu tena Young Killer. Kuhusu Gigy Money kiukweli mimi sikumwita kwenye video yangu, ‘Video Queens’ wote wakifanya kazi yangu huwa nawalipa,” anasema Nay.
POVU KWA DIMPOZ, ALI KIBA, DIAMOND PLATNUMZ
Agosti 23 mwaka huu, Nay wa Mitego kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika maneno ya kuwakosoa wasanii wenzake Ommy Dimpoz, Ali Kiba na Diamond Platnumz kuhusu ugomvi wao ambao alidai ulivuka mipaka.
Rapa huyo ametoa sababu zilizomfanya kuwatukana wasanii hao baada ya Dimpoz kuweka picha mtandaoni akiwa na mama mzazi wa Diamond.
“Nampenda sana mama yangu, unaweza kunitukana mimi na watoto wangu kadri unavyoweza lakini ukimgusa mama huwezi kubaki salama, unajua wakati mwingine unaweza kupata laana, na siyo mzazi wako tu anaweza kukupa laana hata mwanamke yeyote anayejua uchungu wa kuzaa anaweza kukulaani,” anasema Nay.
HAWEZI KUISAHAU HII SIKU
Nay wa Mitego amekuwa mtu wa matukio mengi lakini hapa anaeleza tukio moja ambalo hawezi kulisahau kwenye maisha yake.
“Siwezi kusahau siku nilipokuja kuongea tena na mama yangu, nilikaa miaka mitano bila kuongea na mama yangu, hiyo ilitokana na mambo yangu ya ujana, siku hiyo mama alinipa baraka za kuendelea kufanya muziki,” anasema.
TUKIO LILILOMTOA CHOZI
Mkali huyo wa singo ya Makuzi, anasema tukio ambalo lilimuumiza zaidi mpaka akatoa machozi ni pale mama wa mtoto ake wa mwisho (Curtis) siyo damu yake.
“Wakati huo nilikuwa tayari nimemchukua mtoto kwa mama yake naishi naye, nilishinda siku nne bila kula chochote zaidi ya kunywa juisi, kila nikimwangalia mtoto wangu, Curtis nilikuwa natoa machozi mpaka nilipokwenda kupima DNA, mbaya zaidi nikaambiwa majibu yatatoka baada ya wiki tatu, nilizidi kudata lakini nashukuru majibu yalilipotoka ikaonekana ni damu yangu,” anasema Nay.
UHUSIANO WAKE NA MZEE WA UPAKO
Baada ya Nay wa Mitego kutangaza kujenga kanisa, Februari 21 mwaka huu, Mchungaji Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ aliibuka na kumuonya huku akimtaka aache kufanya hivyo kwani ni kufuru na kumchezea Mungu, msanii huyo anafafanua jambo hilo..
“Ujenzi wa kanisa unaendelea, tumepata eneo na tunaendelea kujenga, watu mbalimbali wamejitokeza kusapoti. Kuhusu Mzee wa Upako nadhani mtu aliyempelekea taarifa alikosea kuiwasilisha ndiyo maana mchungaji akasema vile, lakini nashukuru amelielewa lengo langu na ameahidi kunipa mchango wake,” anasema Nay.
KUTIWA NGUVUNI NA POLISI
Machi 25 mwaka huu Nay wa Mitego alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, ikiwa ni siku chache baada ya kutoa wimbo wake wa Wapo. Nay anasilimulia kitu cha kwanza alichokifanya baada ya kupata taarufa za kutakiwa polisi.
“Nilipogundua kuwa polisi wamezunguka hoteli niliyokuwa nimelala, kitu cha kwanza nilimpigia simu mama yangu, nikamwambia atulie, awe na amani kwani hakuna tatizo lolote litakalonipata,” anasema Nay wa Mitego.
Mtanzania
Comments
comments