NDANI YA BOKSI: Bongo Fleva Inapoishi kwa Matukio
Msimu wa Fiesta unakaribia. Tegemea nyimbo nyingi za Bongo Fleva kuachiwa kipindi hiki. Kwa msukumo wa tukio la Fiesta ili wapate nafasi ya kupanda majukwaani katika mikoa mbalimbali. Shoo zilizokuwa zikiandaliwa na kina Nyau kule Morogoro na mwenzake Ngedere hazipo hivi sasa hata kama zipo siyo kama zamani kimapato na msisimko.
Mdosi wa Shinyanga sidhani kama ana namba ya Young Killer na kina Shilole. Ndivyo ambavyo Kampuni ya 5 Stars Entertainment ya Tanga imetoweka kwenye masikio ya wadau wa Bongo Fleva.
Kusema muziki umekua inabidi utoe ufafanuzi mkubwa. Kinachoendelea ni muziki kutengeneza matukio zaidi huku wasanii wawili watatu wakitanuka na kuacha pengo kubwa la mafanikio kwa wenzao.
Muziki umekua kwa mwanamuziki mmoja kuwa staa pekee kwa mwaka wa saba sasa? Tusidanganyane muziki umekata ringi unaenda kama gari la mkaa, tripu moja porini moja gereji.
Utaniaminisha vipi kuwa muziki umekua kwa kuwatazama wawili tu Dai na Kiba? Ni kama soka la Bongo kutawaliwa na Simba na Yanga tu. Katika ubora wake muziki ulikuwa juu. Watangazaji wa vipindi vya Bongo Fleva redioni walikuwa juu kwa umaarufu ule ule kama wa wanamuziki.
Venture alikuwa staa kama Mr Blue. Steve B alikuwa staa kama alivyokuwa Noorah. Leo hii watangazaji wa vipindi vya umbea kama Shilawadu wanakuwa maarufu kuliko wanamuziki. Ndo maana wanamuziki wa sasa wanawategemea Shilawadu kupeleka umbea ili wazungumziwe kwenye vipindi hivyo kwa mambo ya nje ya muziki.
Muziki umekuwa wa matukio wanategemea matukio ya uhusiano wa kingono na totoz za Bongo Movie ili wapande chati na si ubora wa tungo na sauti.
Wakati zamani watu walikuwa wanatega sikio redioni kusikia wimbo mpya, leo wanatega sikio na macho ili wasikie na kuona muendelezo wa penzi la Wolper na Harmonize. Muziki na wanamuziki wanaishi kwa matukio.
Harmonize anatumia tukio la penzi lake na Jack Wolper ili kuwafanya watu watege sikio juu yake kabla hajaachia wimbo mpya. Na ndo maana wanamuziki wanasubiri msimu wa Fiesta ili waachie nyimbo wapate shavu kwa tukio la Fiesta.
Muziki umeyumba. Huu si wakati wa Bongo Fleva kutamba Afrika kwa jina la mwanamuziki mmoja tu. Tunahitaji kuwa na kina Diamond wa kutosha kwa ubora na kipato kama ilivyo kwa Wanaijeria. Lakini kinachoendelea ni uwepo wa daraja kubwa la kipato na umaarufu kwa Diamond na wenzake. Shoo anazofanya Diamond huko Zambia, Mr Nice alifanya miaka 15 iliyopita. Si kitu kipya. Na maisha ya Nice na Ferouz hayakuwa na utofauti sana kama Diamond na Belle 9 kwa sasa.
Maana yake ni kwamba Ferouz aliishi vizuri kama Mr Nice kwa shoo za ndani ya nchi bila kutoka nje ya mipaka. Sasa mtazame Diamond na Fid Q, ni Vogue na Bodaboda. Tofauti ni kubwa.
Lakini wakati ule Nice alikodi ndege kwenda kwenye shoo Comoro huku Profesa Jay akiendelea na shoo zake za Sitimbi na Makorokochoni vizuri tu. Na maisha yao yalikuwa hayana utofauti kuanzia magari ya kutembelea mpaka bili za pombe kwenye kaunta za klabu za usiku.
Kama mtu utajidanganya kuwa Mr Nice alikuwa analipwa pesa kidogo kwa shoo za nje kuliko Diamond wa leo utakuwa unakosea. Tunamuongelea Mr Nice aliyekwenda Japan badala ya Twanga Pepeta kwenye shoo siyo tafrija ya Wabongo. Tunamuongelea Nice ambaye alipiga shoo Zambia, Malawi, Msumbiji, Uganda, Kenya na Comoro kwa dau la dola elfu 20 kwa shoo mara kwa mara katika utawala wa Mkapa. Ogopa.Ndiyo maana pesa ilimtia uchizi.
Kilichopo ni Diamond kuzichanga karata zake vyema kwenye maisha tofauti na Nice. Bongo Fleva si mtu mmoja au wawili. Ni kitu ambacho kilikuwa kinazalisha ajira ndani ya ajira. Mwenye ukumbi alipata pesa, promota na wasaidizi wake na washereheshaji wa shughuli walipata pesa. Na zaidi kampuni za vinywaji zilipata pesa kupitia muziki huu. Kuna watu mikoani walijenga nyumba kusomesha watoto shule nzuri kupitia muziki huu. Bongo Fleva haikuwa faida kwa wanamuziki tu. Leo hii miaka mingi imetoweka bila msanii kutoa albamu. Ni vipi nikuamini unaponambia muziki unakua? Wenye ‘stationary’ walipata pesa kwa kutengeneza vipeperushi vya shoo na posters. Ndivyo ilivyokuwa kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni. Ulikuwa ukisikia Afande Sele yuko Tabora, Blue yuko Tanga, Daz Baba yuko Kahama na Gangwe Mobb wako Mtwara na Soggy yuko Kilombero. Na wote walijaza watu na kupata pesa.
Hii leo wote hao utasikia wapo Instagram si kwenye shoo. Leo hii wanamuziki wako bize kujibu shutuma kwenye vipindi vya Shilawadu na kuposti vinywaji Instagram.
Wanaishi kwa matukio na kina Nay wa Mitego wanabamba kwa nyimbo za matukio. Roma anaongelewa kwa tukio la kutekwa kuliko kazi yake. Chid Benz anaongelewa kwa tukio la uteja na kutoka rehab muziki wake umewekwa kando. Linah tukio la ujauzito wake ndiyo habari ya mjini na siyo sauti yake. Ndivyo ilivyo kwa Barnaba na tukio la kutelekezwa na mkewe limeuteka muziki wake. Muziki wa Bongo Fleva uko pale pale ila akili ya Diamond imejiongeza.
Kusema kuwa muziki huu umekua kwa ubora, umaarufu na mafanikio ya Diamond ni sawa kabisa na kumtazama Champion Boy Mbwana Samatta na kusema soka la Bongo limepanda wakati bado linaendeshwa kwa kamati za saa 72 huku timu ikililia pointi za mezani.
Diamond anaenda kuchukua tuzo nje ya nchi. Kwenye korido akitazama kushoto anamuona Sallam. Kulia Mose Iyobo. Wakipishana na wanamuziki wa Kinaijeria kibao. Tunawahitaji kina Diamond wa kutosha badala ya kutuletea stori za Baraka Da Prince na Naj. Muziki na wanamuziki wahame kwenye matukio. Mwenye mawasiliano na Asha Baraka, Ally Choki na Nyoshi wapeni salamu. Muziki unaishi kwa matukio hivi sasa.
By Dk Levy. Mwananchi