Artists News in Tanzania

Nimezaliwa Upya, Subirini Cheche!-TID

VITA vya dawa za kulevya imeshika kasi huku tukiona wasanii wakizungumziwa kutokana na kujihusisha na matumizi ya dawa hizo.

Matumizi ya dawa za kulevya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ndoto za watumiaji. Watumiaji katika jamii ni wengi huku sanaa ikiwa ni moja ya wahanga wakubwa wa tatizo hilo.

Ni rahisi kuwatambua wasanii wanaojiusicha na matumizi au kufanya biashara haramu kwenye jamii kwani wao ni  maarufu na kioo cha jamii.

Hayo yamejitokeza hivi karibuni baada ya Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul  Makonda, kutaja majina ya watu mashuhuri wanaodaiwa kujihusisha na biashara na kutumia dawa za kulevya.

Staa wa Bongo Fleva kutoka kitambo, Khaleed Mohamed ‘TID’ au Mnyama ni miongoni mwa waliotajwa kuhusika na utumiaji wa dawa za kulevya.

Polisi wa Swaggaz alimsaka staa huyo na kufanikiwa kukutana naye ambapo alitoa ushirikiano wa kutosha katika interview iliyofanyika pande za Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Hapa chini ni sehemu ya mahojiano hayo.

SWAGGAZ: Ni kweli ulikuwa unatumia dawa za kulevya?

T.I.D: Ni kweli nilikuwa mtumiaji wa dawa hizo lakini kwa sasa nimebadilisha mfumo wa maisha yangu na kuwa mtu mpya ambaye ni T.I.D mpya.

SWAGGAZ: Je, baada ya kuwa mtumiaji wa dawa hizo ni  kitu gani unajutia zaidi?

T.I.D: Nimepoteza fedha nyingi kutumia kwenye masuala ya dawa  kwani hizi sasa ningekuwa tajiri, nimefanya sterehe nyingi bila kujua. Kwakweli najutia sana.

SWAGGAZ: Umejifunza nini kupitia sakata hili?

T.I.D: Ni kitu cha kumshukuru Mungu kwani nimejifunza mengi kupitia sakata hili kwa sasa nafuatilia kazi zangu kwa umakini na nina muda wa kutosha kwa kufanya kazi na wasanii wezangu.

Namshukuru sana Mkuu wa Mkoa, Makonda kwani bila ya kampeni hii sijui ningekuwa wapi sasa hivi! Lakini mimi nashukuru zaidi kwa kuweza kuachana na hayo madawa, sasa naishi maisha mapya. Mashabiki wangu wasubiri cheche za T.I.D, mzee wa Zeze.

SWAGGAZ: Mashabiki wategemee nini kutoka kwako?

T.I.D: Kama nilivyosema awali, nimerudi tena kwa kasi ya ajabu kwani kuna kazi nyingi mpya zinakuja kutoka kwangu ikiwemo wimbo wangu mpya wa Maisha ya Jela na filamu ya sehemu ya pili ya Girfriend. Nadhani wadau wanaikumbuka.

SWAGGAZ: Vipi maonyesho na bendi yako ya T Band?

T.I.D: Bendi ipo na kutokana na matatizo yaliyonikuta ndiyo yamefanya bendi hiyo kutosikika lakini kwa sasa nimerudi na kila kitu kitakaa sawa.

Mashabiki zangu na wapenzi wa kazi za bendi wakae mkao wa kula kusikia vitu vipya kutoka kwenye bendi yetu.

SWAGGAZ: Ni maisha gani umekutana nayo wakati ukiwa mahabusu?

T.I.D: Mahabusu ni mahabusu tu hakuna maisha mazuri kwani kulala kwa muda wa kupangiwa na kuishi maisha bila uhuru ni mabaya, sijapenda… siwezi kupenda maisha ya kule hata siku moja. Sitamani kurudi tena kule kabisa.

SWAGGAZ: Unawapa ushauri gani vijana ambao bado wanatumia dawa za kulevya?

T.I.D: Maisha yamebadilika, vijana tunatakiwa kuwa nguvu kazi ya Taifa na kuacha kufanya vitu visivyokuwa na maana kwani utumiaji wa dawa za kulevya unapotosha vijana na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Hakuna faida yoyote ya kutumia dawa za kulevya zaidi na kutumia muda mwingi kuwa teja na fedha nyingi kwenye manunuzi za dawa hizo.

SWAGGAZ: Unatoa ushauri gani kwa wasanii chipukizi wanaotaka kuingia kwenye muziki kwa sasa ni vitu gani wazingatie?

T.I.D: Wasanii chipukizi wanatakiwa kuwa wabunifu zaidi kwani kwa sasa sanaa imekuwa ngumu na wasanii wanaongezeka kila siku, pili kuwa na nidhamu ya kazi na kuacha kujiingiza kwenye mambo yasiyo na maana.

SWAGGAZ: Kwa sasa umejipangaje kwa ajili ya kupambana dhidi ya utumiaji ya dawa za kulevya?

T.I.D: Nimejitolea kuwa balozi wa vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Na BEATRICE KAIZA, Mtanzania

Comments

comments

Exit mobile version