MSANII wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Nuh Mziwanda ambaye jina lake la kuzaliwa ni Naftal Mlawa, ni mmoja kati ya vijana wanaofanya vizuri katika ulimwengu wa Bongo Fleva kwa sasa.
Miaka michache iliyopita, jina lake lilikuwa kubwa katika vyombo mbalimbali vya habari, lakini si kwa muziki, bali kwa uhusiano wake wa kimapenzi uliopata umaarufu akiwa na msanii mwen-zake, Zuwena Mohamed ambaye jina lake la kisanii ni Shilole a.k.a Shishi Baby.
Na walipata kujulikana sana kwa sababu ya uwepo wa madai kuwa Nuh alikuwa mdogo kiumri kuliko Shilole ambaye mara kadhaa alikuwa akimtetea mpenzi wake huyo kwa kudai alikuwa sawa naye.
Hata hivyo baadaye wawili hao waliachana na kila mmoja kuchukua ‘time’ yake na maisha yakaendelea. Juzikati, Nuh alikutana na Risasi Vibes na kupiga stori mbili tatu.
Risasi Vibes: Tuanze na kazi yako ya muziki, unamiliki studio, Last Born Records, vipi utendaji wake kwa sasa na je, una wasanii?
Nuh: ‘Ofcoz’ wasanii wapo tena wako mbioni kutoa track zao na wakiwa tayari nitaweka wazi, lakini upande wa studio inaendelea vizuri kwa sababu kwa sasa imefanya ngoma kubwa tatu ambazo ni Anameremeta, Bao la Ushindi na wimbo wa Ali Kiba ambao unahusu kampeni za huko Kenya.
Risasi Vibes: Baada ya ujio wako wa sasa wa Bao la Ushindi, kuna ‘project’ nyingine ambayo unaweza kuizungumzia?
Nuh: Hapana, acha Bao la Ushindi isumbue kwanza kwenye gemu, maana bado inafanya vizuri.
Risasi Vibes: Katika ‘plan’ zako za baadaye kuna msanii yeyote wa nje ambaye unatamani kushirikiana naye kwenye kazi?
Nuh: Hapana. Ninapohitaji kufanya kolabo huwa siplan, lakini naangalia wimbo ninaotaka kufanya unamtaka nani, na yule ambaye atafiti bila kujali yupo ndani ya nchi ama nje nitamshirikisha.
Risasi Vibes: Mbali na kazi, kuhusu maisha yako binafsi, tangu uachane na mkeo maisha yanaendaje?
Nuh: Safi tu, ninafurahia maisha kama kawaida.
Risasi Vibes: Na vipi kuhusu malezi ya mtoto, anaishi na nani na mawasiliano kati yenu na mzazi mwenzako yapoje?
Nuh: Mtoto anaishi na mama yake. Lakini huwa ninawasiliana naye katika hali ya kufahamu anaendeleaje. Na kiukweli nipo bega kwa bega na mwanangu.
Risasi Vibes: Hata hivyo kuna wasomaji ambao mpaka sasa hawafahamu sababu ya wewe na mkeo kuachana, wengine wanadai kwamba Shilole ndiye alisababisha ndoa yako ikavunjika, kuna ukweli wowote kwenye haya?
Nuh: Hapana, Shilole hajahusika na lolote lile mimi kuachana na mama mtoto wangu. Sema kama ujuavyo Watanzania, wao wape picha tu, kepsheni wataandika wenyewe.
Walipokuwa wananiona na Shilole pengine kwenye shoo au sehemu yoyote ile wao wanaunga doti kwamba tunatoka, lakini si kweli.
Risasi Vibes: Kipi hasa ni sababu kubwa ya wewe kuachana na mzazi mwenziyo?
Nuh: Wazazi wake. Kwa sababu ambazo mpaka leo sijazielewa lilitoka shinikizo ndani ya familia yake kwamba niachane naye. Kwa hiyo yeye pia aliwasikiliza wazazi wake akaamua kuolewa na mtu mwingine.
Risasi Vibes: Siyo kwamba mlikuwa na tofauti zozote?
Nuh: Hapana.
Risasi Vibes: Pia hamkuzu-ngumza zaidi juu ya hili kabla hajaolewa kwingine?
Nuh: Tulizungumza sana, lakini wazazi walikuwa na nguvu kuliko mimi.
Risasi Vibes: Ikitokea leo akarudi na kukuomba msamaha kwa yote na kukutaka mrudiane, utakubali?
Nuh: Siwezi kukubali. Sifikirii kurudiana naye, siwazi na wala sitamani. Hiyo ilikwishapita, itabaki historia.
Risasi Vibes: Umekuwa kwenye uhusiano na staa, baadaye mtu wa kawaida, kwa sasa unahitaji mwanamke wa namna gani?
Nuh: Kwa sasa nipo ‘single’, sijafikiria wala kuhitaji mwanamke, bado akili yangu nahitaji itulie kwanza.
Risasi Vibes: Asante sana kwa ushirikiano wako, labda mwisho una lolote kwa mashabiki wako?
Nuh: Niwatake wazidi kunipa sapoti zaidi. Video ya Bao la Ushindi ndiyo hiyo nimeachia Ijumaa, wategemee kazi nzuri zaidi kutoka kwangu.
Ukiachana na ngoma zake zilizowahi kutamba hapo nyuma kama Jike Shupa na Aname-remeta, kwa sasa wimbo wake wa Bao la Ushindi unaki-mbiza kwenye chati mbali-mbali.
Chanzo:GPL
Comments
comments