Rammy Galis:Nilikaribishwa Freemason Nikakataa
Star wa Bongo Movie Rammy Galis amefunguka na kukiri kuwa kuna watu hususani wasanii wanaojihusisha na kundi la Freemason na kwamba yeye mwenyewe aliwahi kualikwa kwa njia ya simu yake ya mkononi ajiunge na kundi hilo lakini alikataa.
Akizungumza katika kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa LIVE kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, Galis amesema yeye hajajiunga na Freemason na wala hatafanya hivyo lakini alishawahi kutumiwa ujumbe wa kujiunga.
Galis alikuwa akijibu swali kutoka kwa mmoja ya mashabiki wake aliyetaka kujua iwapo Diamond pia yupo katika kundi la Freemason au illuminati kama ilivyokuwa ikidaiwa kwa marehemu Steven Kanumba, ambapo alisema kuwa yeye hawezi kufahamu, na kukiri kuwa suala hilo kwa wasanii lipo na ni la kawaida.
“Kwa kuwa nimeulizwa, ngoja nijibu, ukweli kuna siku nilipata meseji kama ilivyo kwa ujumbe wa tigo pesa au M-Pesa, iliyokuwa na kichwa kilichosomeka Freemason, ujumbe huo ulinitaka nijiunge na Freemason, kama niko tayari kujiunga na biashara hiyo nijibu ujumbe huo na kama sitaki nifute ujumbe huo, nilipojaribu kufuatilia zile namba zikaonesha kwamba hazitambuliki (Unknown number), basi nikaufuta na wala sijafuatilia tena, kwahiyo kuhusu Diamond, mimi sijui” Amesema Galls
Aidha msanii huyo amesema anatarajia kuachia filamu kali mwezi Desemba mwaka huu na kuwataka wananchi kumuunga mkono kwani itakuwa na ubora wa hali ya juu na kwamba ameitengenezea nje ya nchi na wasanii wakubwa wa Nigeria.
Pamoja na hayo Rammy Galis amewataka wasanii wa Bongo Movie kukaza katika soko la sasa na kuto kata tamaa kwani mafanikio hayaji bure bila kuweka juhudi za makusudi .