Riyama Ally ‘Mkegani’ Awachana Maproducer Miyeyusho
Msanii mahiri wa filamu Tanzania Riyama Ally anayetambulika kwa sasa kama malkia wa uswazi au Mkegani amewalalamikia watayarishaji wa filamu nchini kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuua vipaji vya wasanii hapa nchini.
Wasanii wamekuwa wakijadiliwa na kukosolewa sana katika uigizaji wao na kutobadilika kuendana na husika wanazocheza katika filamu. Leo nimepata fursa ya kuongea na mmoja wa wasanii wanaofanya vizuri sana sokoni, Riyama Ally ambaye
amepachikwa taji la umalkia wa uswahilini na mashabiki wake, Riyama anazungumziaje hali hiyo?
“Tatizo kubwa ni watayarishaji kaka yangu, watayarishaji wengi wanapenda kuandika script wenyewe au wanawapa kazi watu wao wa karibu wakati hawana utaalamu wa kuandika, matokeo yake inabidi msanii ajiongeze sana ili aweze kuigiza vizuri na kulinda hadhi yake kwa mashabiki, matokeo yake ndio utakuta mtu anacheza kile kile katika filamu zote.” Alifunguka Riyama.
Pia alitaja sababu nyingine ni watayarishaji kuwa na woga wa mabadiliko. Watayarishaji wakiona msanii amecheza vyema katika husika moja ya mtayarishaji mwenzao basi kila mtu atataka ukaigize filamu yake kwa husika hiyo hiyo hata kama hadithi haitaki hivyo.
“Mfano zamani kila producer akija anataka nicheze sehemu za kulia hadi nikaitwa mama wa kulia lia. Nikacheza kipande cha mcharuko sasa kila mtayarishaji anayekuja anataka ucheze mcharuko. Namna hii ni lazima kipaji chako kiwe hatarini.”
Mwandishi alipombana kuwa ni kwanini wasikatae kuigiza endapo mtayarishaji atawaitia kazi ambayo haina script ya kueleweka, Riyama alitiririka
“Kazi yetu ni kuigiza na asilimia kubwa ya watayarishaji wako hivyo, ukiwagomea utaigizia wapi? Tasnia ya filamu Tanzania bado sana. Tunahitaji elimu sana na kanuni za kutuongoza zenye kuzingatia mambo ya msingi kama haya
,”
“Tasnia hii ishawahi kutokea nimekubaliana kufanya kazi na producer, akanichezesha scenes kumi halafu akamuuzia mwenzake scene tatu ili huyo mwenzake aweke kwenye filamu yake apate sababu ya kuniweka kwenye kava. Haya maajabu sijui kama yameshawahi kutokea katika nchi nyingine”
Akizungumzia ujio wa filamu ya Mkegani ambayo imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii, Riyama aliahidi wapenzi wake kumuona Riyama Ally aliyetulia katika script iliyoandikwa kitaalam.
“Watamuona Riyama wa tofauti kwa vile nimefuata script na maelekezo ya Director na ndicho kitu ambacho napenda,” alibainisha Riyama.
Akizungumzia wasanii ambao wanatayarisha wenyewe filamu zao halafu wanacheza husika zile zile, Riyama alisema kuwa wasanii hao wanakosa kujiamini katika kazi yao ya uigizaji hivyo wanawalazimisha waandishi wawaandikie filamu zinazoendana na wao hivyo kuwanyima waandishi nafasi ya kufanya ubunifu.
“Lakini madhara yake tumeshaanza kuyaona kwani baadhi yao wameanza kukataliwa sokoni na wasipofanya juhudi ya kubadilika ili kuwapa mashabiki wao ladha mpya watajiua wenyewe” alishauri malkia huyo wa uswazi.
Akielezea husika yake katika filamu ya Mkegani, Riyama alisema tu kwa kifupi kuwa ameigiza kama mwanamke aliyekumbwa na mabalaa ya kuachika.
Filamu hiyo ya Mkegani iliyoandikwa na kuongozwa na Ignas Mkindi inatarajiwa kuleta msisimko mpya katika tasnia ya filamu kutokana na kuigizwa na wasanii kibao wakongwe na maarufu kama Muhogo Mchungu, Bi Star, Sulemani Barafu, Haji Mboto, Baba James, Seif Mbembe, Bi Hindu na wengineo wengi.
FC