Artists News in Tanzania

Shahidi: Wema alinieleza anatumia bangi kama starehe

Shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, WP 6441 DC Mary (35) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu alimueleza kuwa anatumia bangi kama starehe.

Shahidi huyo amedai hayo leo Februari 26, 2018 wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mary amedai kuwa Februari 4, 2017 alipewa maelekezo na mkuu wake wa kazi OC CID, Denis Mujumba kumtoa Wema mahabusu na kwenda nyumbani kwa msanii huyo kufanya upekezi.

Amedai kuwa alimtoa msanii huyo mahabusu na kuondoka naye katika gari wakiwa yeye, OC CID Mujumba, Inspekta Wille, Koplo Robert na DC Hassan kuelekea nyumbani kwa Wema, Bunju Basihaya.

Amedai kuwa wakiwa njiani alimueleza Wema kuhusu tuhuma zinazomkabili kuwa anahusika na uuzaji wa dawa za kulevya ama kutumia.

Shahidi huyo ameeleza kuwa baada ya kumueleza Wema hayo, alisema yeye hajishughulishi na uuzaji Ila anatumia bangi kama starehe.

Amedai kuwa alimuuliza Wema kuwa ni lini ilikuwa mara ya mwisho kutumia bangi na kwamba, siku hiyo ilikuwa Jumamosi ya Februari 4, 2017.

Wema alimwambia kuwa mara ya mwisho kutumia bangi ilikuwa siku ya Jumatatu.

Marya amedao kuwa wakati huo walikuwa njiani na walipofika nyumbani kwa Wema waligonga geti na likafunguliwa na mfanyakazi wakaingia ndani na walimkuta mfanyakazi mwingine wa msanii huyo.

Amedai kuwa kabla ya upekuzi Wema aliomba dada yake Nuru Sepetu apigiwe simu ili awepo katika upekuzi, akapigiwa akafika pamoja na mjumbe Steven Ndoho naye aliitwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 12 na 13, 2018 ambapo mashahidi wataendelea kutoa ushahidi dhidi ya Wema na wenzake.

Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Februari 4, 2017 katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio, washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Kwa upande wa Wema yeye anadaiwa kuwa Februani Mosi, 2017 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Wema ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Inadaiwa kuwa Februari 3, 2017, Wema alijipeleka mwenyewe katika Kituo cha Polisi Kati ambapo alikamatwa.

Mwananchi

Comments

comments

Exit mobile version